Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akisisitiza jambo
wakati akiongea na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma
(hawapo kwenye picha)
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akiteta jambo na
Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe, wakati alipofanya
ziara ya kuongea na Watumishi wa Sekta ya Afya katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Baadhi ya Watumishi kutoka
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakifuatilia neno kutoka kwa Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin
Mollel pindi alipofanya ziara katika Hospitali hiyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akimjulia hali mtoto
aliefika na mzazi wake kupata matibabu katika wodi ya watoto, Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akimjulia hali mama
aliyempeleka mtoto kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma.
Jengo la Idara ya magonjwa ya wanawake na uzazi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
******************************
Na WAMJW- DOM
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amewashukuru
Watumishi wote wa Sekta ya Afya nchini kwa namna walivyojitoa katika
mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Dkt. Mollel ameyasema hayo leo,
wakati alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi wa Sekta ya Afya katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Rufaa ya kanda ya
kati ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
“Jinsi ambavyo nyie mmepambana
dhidi ya virusi vya Corona na bado mkamuunga mkono Mhe. Rais na ushauri
alioutoa yeye na Wataalamu wengine wa Wizara , nyie mmekuwa mashujaa na
jeshi la uzalendo wa hali ya juu, nawashukuru sana” alisema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel aliendelea kwa kukemea
tabia za watu wa nje ya nchi na baadhi ya Watanzania wachache kupotosha
Watanzania na Dunia kwa ujumla juu ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa
Corona kwa Watumishi wa Sekta ya Afya nchini jambo ambalo sio kweli.
“Kuna wenzetu wako huko nje
wanapiga kelele kuhusu Corona kuliko sisi, nawaomba watu tuache kupiga
siasa, kama kweli kuna Watumishi wanakufa kwa Corona kama wanavyosema
niliwaambia waende hospitali Dodoma waulize idadi ya Watumishi
waliokuwepo kabla ya Corona kisha waulize waliopo sasa” alisema.
Aidha, Dkt Mollel alitoa wito kwa
Watumishi wa Sekta ya Afya nchini kufanya kazi kwa bidii katika
kuwahudumia wananchi ili kutoa huduma bora, huku akiweka wazi kuwa kazi
ya kuwahudumia wananchi ni ya wito na ya uzalendo.
Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest ameweka wazi kuwa
Hospitali hiyo imeendelea kutoa huduma za Afya bila kutetereka na kutoa
elimu kwa umma licha ya kupitia katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya
Corona ulioikumba nchi.
“Tumeendelea kutoa huduma bora kwa
wananchi bila kutetereka hata katika wakati huu wa janga la mlipuko wa
maambukizi ya virusi vya Corona ulioikumba nchi, Watumishi wetu
wamesimama imara huku wakiendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya
Corona “alisema.
Aliendelea kusema kuwa, licha ya
mafanikio ambayo hospitali hiyo imeyapata suala la ucheleweshwaji wa
upatikanaji wa fedha zinazotokana na makusanyo ya ndani kwaajili ya
uendeshaji wa shughuli za Hospitali, hali inayoathiri baadhi ya huduma
katika Hospitali hiyo.
Aliendelea kusisitiza kuwa,
ukosefu wa baadhi ya mashine kama CT scan na MRI umefanya Hospitali hiyo
kuwakosa wagonjwa wengi ambao wanalazimika kwenda Hospitali nyingine
kutafuta huduma hizo, hali inayopelekea kupoteza mapato ambayo
wangeyapata kama huduma hizo zingekuwepo.
“Tunaukosefu wa baadhi ya mashine
za uchunguzi kama vile CT scan na MRI hivyo wagonjwa ambao wanaweza
kutibiwa ndani ya hospitali imetufanya tuwapeleke Hospitali nyingine
kwaajili ya kupata vipimo hivyo kisha kurudi kupata matibabu ” alisema.
No comments:
Post a Comment