Baadhi
ya wafanyakazi waliopoteza ajira wakifuatilia fao la kukosa ajira ambao idadi
yao kubwa ni vijana nguvukazi.
.
Na Christian Gaya
Majira Ijumaa 29 Mei 2020
Fao la Upotevu wa ajira
limo kwenye sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa
Umma (PSSSF)
ya mwaka 2018 na kwenye Mfuko wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Agosti
Mosi, mwaka 2018, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),
ulianza rasmi ukiwa ni utekelezaji wa Sheria Namba 2 ya 2018, ambayo pamoja na
mambo mengine, iliunganisha mifuko ya pensheni minne ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF
na kuunda mfuko mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma yaani PSSSF.
Sambamba na kuanzishwa
kwa PSSSF, sheria hii ilifanya marekebisho kwenye sheria ya Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii (NSSF) Sura ya 50 ili kuufanya mfuko wa NSSF kuwa
utakaohudumia wafanyakazi wa sekta binafsi na sekta isiyorasmi.
Ili kukabiliana na tatizo
hilo la wanachama kujitoa katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii pamoja na
kukidhi mahitaji ya mfumo wa hifadhi ya jamii wa kuwa na utaratibu wa kinga ya
kipato kutokana na upotevu wa ajira, Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii (SSRA) wakati huo kabla ya kuvunjwa rasmi, ilikuja na mapendekezo ya
kuanzishwa kwa fao la upotevu wa ajira.
Fao hili la upotevu wa
ajira litatolewa kwa wafanyakazi ambao ni wanachama wa mifuko ya hifadhi ya
jamii pale wanapopoteza ajira zao.
Fao hili linatokana na
mchango wa pensheni wa mwanachama kumwezesha kujikimu katika kipindi
anachotafuta ajira nyingine.
Ikitokea
mwanachama huyo hajapata ajira nyingine miezi 18 baada ya kupokea malipo ya
kutokuwa na ajira basi atatakiwa kubadili michango yake kwenda mpango wowote wa
kuchangia kwa hiyari aupendao.
Kiwango
kinachohamishwa kwenda mpango huo kinakuwa jumla ya michango yote kutoa
pensheni aliyolipwa kipindi cha kukosa ajira. Mwanachama huyo ataendelea
kuchangia mpango aliouchagua kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazousimamia.
Utaratibu
wa fao la kukosa ajira linawahusu wale wanaofanya kazi za muda mfupi au za
mkataba pia.
Wafanyakazi wanaopoteza
ajira wameanza kunufaika na fao la upotevu wa ajira katika mifuko ya hifadhi ya
jamii baada ya mifuko hiyo kutangaza kuanza kupokea maombi tangia mwaka mwanzoni
2019.
Tunafahamu
kwamba fao la kukosa ajira halitolewi kama msaada, bali lipo kwenye sheria mpya
ya mifuko ya hifadhi ya jamii na kuunganishwa kwa baadhi ya mifuko hiyo, hivyo
wana haki kabisa ya kulipwa kama ilivyoelekezwa.
Fao la upotevu wa ajira
ni jipya lililoanzishwa baada ya kuwapo kwa kilio cha muda mrefu cha
wafanyakazi kutaka kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii wanapoacha kazi.
Uanzishwaji wa fao hili
unawezesha kutekelezwa na kuimarishwa kwa dhana ya hifadhi ya jamii kwa
kuwajali wafanyakazi wanaopoteza ajira kwa kuwawekea kinga ya kipato itakayo
wawezesha kupata fedha za kujikimu katika kipindi wanachotafuta kazi.
Faida nyingine kuwa ni
kuondoa migogoro ya kikazi na malalamiko ya wafanyakazi yaliyopo kutokana na
kuwepo utaratibu unaokubalika na hivyo kuongeza ari na tija sehemu za kazi.
Fao la upotevu wa ajira inaimarisha
mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kupunguza matumizi ya fedha ya kuwalipa
wanachama wanaoamua kujitoa kwenye mifuko bila sababu za msingi na kisha kuwa
mzigo kwa jamii na serikali hapo baadaye.
Utaratibu huu hautakuwa
na gharama kwa serikali kwa sababu fedha za malipo ya fao la upotevu wa ajira
zitatokana na michango ya pensheni ya mwanachama mwenyewe.
Kabla ya fao hili jipya,
kilio cha wafanyakazi wengi waliokuwa wanapoteza kazi ilikuwa ni kujitoa katika
mifuko ya hifadhi ya jamii kiasi cha kuwapo kwa dhana kwamba lipo fao la kujitoa.
Hivyo, kutokuwepo kwa
utaratibu mbadala wa kujipatia kipato mara baada ya kupoteza ajira kulisababisha
baadhi ya wafanyakazi kudai kulipwa michango yao ya pensheni.
Kwa mujibu wa takwimu,
wafanyakazi walio kwenye kundi la masharti ya ajira za kudumu ndio lina matukio
mengi ya wanachama kujitoa.
Kwa mfano katika kipindi
cha Julai 2016 hadi Disemba 2017, kati ya wanachama 23,000 waliojitoa kwenye Mfuko
mmoja wa hifadhi ya jamii iliyokuwa sawa sawa na asilimia 78.3 sawa na
wanachama 18,000, walikuwa wafanyakazi walio kwenye masharti ya kudumu.
Wafanyakazi 5,000 sawa na
asilimia 21.7 walitokana na kundi la wafanyakazi walioajiriwa kwa mikataba ya
muda mfupi na ambao hawana ujuzi mkubwa walioajiriwa kwenye mashamba, migodi na
miradi mbalimbali ya muda mfupi.
Kanuni ya mpya mafao ya
hifadhi ya jamii ya mwaka 2018, imebainisha kuwa mafao ya upotevu wa ajira
yatakuwa sawa na asilimia 33.3 ya mshahara wa mwezi wa mwanachama aliyepoteza
ajira.
Sheria
hiyo inautaka mfuko husika kushughulikia maombi ya mwanachama ndani ya wiki
sita, baada ya kukamilisha atakuwa anapewa asilimia 33.3 ya mshahara wake wa
mwisho kwa kipindi cha miezi sita.
Aidha, mafao haya yanatakiwa
kulipwa kwa kipindi kisichozidi miezi sita kwa mwaka na mwanachama anatakiwa
kulipwa kwa kipindi kisichozidi miezi 18 katika kipindi chote cha ajira.
Kama mwanachama atakuwa
hajapata ajira baada ya miezi 18 anaweza kumwandikia mkurugenzi mkuu wa mfuko
huo kuomba kuhamisha michango yake kwenda kwenye mfuko wa hiari wa chaguo lake
na anaweza kuendelea kuchangia katika mfuko huo.
Mwanachama akiacha kazi
kwa hiari yake hatapata mafao hadi atakapofikisha umri wa kustaafu kisheria.
Atashauriwa kuendeleza uchangiaji wake akiwa kwenye ajira nyingine. Kama akiwa
ameachishwa kwa sababu nyingine yeyote bila hiari yake, Mfuko utamlipa mafao ya
kukosa ajira kwa kipindi cha miezi 6, mafao hayo yatasita endapo atapata kazi
kabla ya kuisha kwa miezi hiyo sita.
lkipita miezi 18 baada ya
kwisha kipindi cha kupata fao la kukosa ajira, mwanacharma anaweza kuomba
michango yake kwenye mfuko kuhamishiwa kwenye Mfuko wa hiari. Michango
itahamishwa baada ya kuondoa jumla ya fao la kukosa kazi. Fao la kukosa kazi
litalipwa si zaidi ya mara tatu katika utumishi wote wa wanachama.
No comments:
Post a Comment