Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiteta na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu, Bungeni jijini Dodoma, Aprili 30, 2020. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu).
******************************
NA WAMJW Dodoma
Wizara ya Afya,
kupitia Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii inatarajia kutumia Jumla ya
shilingi bilioni 33.195 ili kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii
hususani zilizopewa kipaumbele kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Akiwasilisha
Hotuba ya Wizara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika mwaka wa fedha 2020/21 Idara
Kuu ya Maendeleo ya Jamii inatarajia kutumia kiasi hicho cha fedha kwa
lengo la kuimarisha huduma na mafunzo kwenye Taasisi za Ustawi na
Maendeleo ya Jamii, kukarabati makazi ya wazee, kujenga mahubusu za
watoto na kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Alisema kuwa
bajeti hiyo itasaidia kuimarisha Kujenga kumbi pacha na hosteli katika
Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo jumla ya shilingi bilioni
2.7 zimetengwa, pia kuboresha utoaji wa mafunzo ya taaluma ya maendeleo
ya jamii ili kukidhi mahitaji ya soko sambamba na kukuza ujuzi wa
wahitimu ikiwemo kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa kutenga
jumla ya shilingi bilioni 6.6.
Maeneo
mengine yaliyotengewa fedha ni pamoja na ukarabati wa majengo na
miundombinu katika makazi ya wazee kwa shilingi milioni 400, ujenzi wa
Shule ya Maadilisho katika Mkoa wa Geita shilingi milioni 200,
kuimarisha ujenzi wa mahabusu ya watoto katika mikoa ya Kigoma na
Mtwara shilingi milioni 700 na kuwezesha Taasisi ya Ustawi wa Jamii
kuboresha utoaji wa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko shilingi
milioni 250.
Aidha, jumla ya shilingi milioni 827.95 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.
“Ili
kutekeleza vipaumbele vilivyoanishwa kwa mwaka 2020/21, Wizara kupitia
Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii imekadiria kutumia kiasi cha shilingi
bilioni 33 kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya Wizara ikiwa
ni pamoja na uendeshaji wa ofisi na miradi ya maendeleo” alisema.
Mhe. Ummy
amesema Wizara imeendelea kukuza ari ya jamii kushiriki katika kujiletea
maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kutumia nguvu kazi na rasilimali
zinazowazunguka na kusimamia masuala yote ya ushirikishwaji wa jamii
kwenye sekta mbalimbali.
No comments:
Post a Comment