…………………………………………………………………………………………………………
Waandishi wa habari
watatu nchini Tanzania, ambao pia ni wamiliki wa runinga mtandaoni, leo
Machi 04, 2020 wamefikishwa kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe,
ambapo kila mmoja anakabiliwa na shitaka moja la kuweka maudhui
mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA).
Waandishi hao, ambao
tangu kukamatwa kwao walinyimwa haki ya dhamana ni; Prosper Daudi
Mfugale, ambaye ni mwandishi wa kituo cha runinga cha ITV na mmiliki
binafsi wa runinga ya mtandaoni ya Njombe TV.
Mwandishi mwingine ni
Ibrahim Godfrey Mlele, ambaye mwandishi wa kituo cha runinga cha TV E
na mmiliki wa runinga ya mtandaoni ya Mlele TV, pamoja na mwandishi
Dickson Kanyika, ambaye anafanya kazi na kituo cha runinga cha Star TV
na kumiliki runinga yake mtandaoni inayojulikana kama Habari Digital TV.
Mbali na waandishi
hao watatu, mtu mwingine aliyekamatwa pamoja na waandishi hao na
kufikishwa mahakamani hapo leo ni Benedict Kisawa, ambaye ni mmiliki wa
runinga mtandaoni inayofahamika kama Njombe Yetu TV.
Wakiwa mbele ya
mahakama hiyo leo, waandishi hao watatu pamoja na mmiliki huyo mmoja wa
runinga mtandaoni kila mmoja amesomewa shitaka lake na kupangiwa hakimu
wake atakayesikiliza kesi yake.
Hata hivyo, waandishi
wote watatu pamoja na mmiliki huyo wa runinga wameshtakiwa kwa kosa
linalofanana, ambapo wamedaiwa kuchapisha habari mtandaoni bila ya kuwa
na leseni kutoka TCRA.
Kwa mujibu wa kifungu
namba 130 (1) cha Sheria ya Mawasiliano ya Mtandaoni na Posta Sura ya
306 (Toleo la Mwaka 2017) pamoja na kanuni ya 14 (1) na 18 ya Kanuni za
Mawasiliano ya Mtandaoni na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) za mwaka 2018
ni kosa kutoa taarifa mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka TCRA.
Mtandao wa Watetezi
wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambao hutetea wanaharakati wa haki
za binadamu nchini humo wakiwemo wanahabari umelaani vikali kitendo cha
wanahabari hao kukamatwa, ambapo umedai kuwa kimsingi kitendo hicho
kinalenga kuendelea kuminya haki ya uhuru wa watu kujieleza kwa kutumia
njia yoyote ikiwemo mitandao.
Mwaka 2018 Mtandao
huo wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania ukishirikiana na
Baraza la Habari Tanzania (MCT) pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu Tanzania (LHRC) ulifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania
ukipinga kanuni za Maudhui ya Mtandaoni kwa madai kuwa kanuni hizo, kwa
kiwango kikubwa zinaminya uhuru wa watu kujieleza, jambo ambalo ni
kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
1977.
No comments:
Post a Comment