Katibu Mkuu Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko
akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar,
Khalfan Sheikh Saleh, wakati akimueleza namna Wakala unavyotekeleza
majukuu yake wakati alipotembelea Wakala huo, Maruhubi, Zanzibar.
Katibu Mkuu Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko akiongea
na baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar, ,
wakati alipotembelea Wakala huo, Maruhubi, Zanzibar.
Mmoja wa Watumishi wa Wakala wa
Uchapaji wa Serikali Zanzibar, akiendelea na shughuli za Uchapaji kwa
kutumia mashine ya Kidigitali kwenye kiwanda cha Wakala huo.
********************************
Na. OWM, ZANZIBAR
Katibu Mkuu Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko ameeleza
kuwa Katika kuhakikisha kuwa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali
inakidhi mahitaji ya
wateja wake kwa kuzingatia ubora wa huduma,
ameitaka idara hiyo kuwekeza kwenye matumizi ya mashine za kidigitali
ambazo zina uwezo wa uchapaji kwa kasi kubwa, viwango bora na kwa idadi
kubwa ndani ya muda mfupi.
Akiongea mara
baada kutembelea Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar kwa lengo la
kujionea namna Wakala inavyotekeleza majukumu yake, Katibu Mkuu Mwaluko
amefafanua kuwa amevutiwa na utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa kuwa
inaendesha shughuli za uchapaji kibiashara, inao usimamizi mzuri wa
ubora unaozingatia teknolojia ya kisasa ya uchapaji, hivyo Idara ya
Mpiga chapa Mkuu wa serikali ya Tanzania bara, hainabudi kutekeleza
majukumu yake kama ilivyo kwa Wakala.
Kwa upande wake
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar, Khalfani
Sheikh Saleh, amefafanua kuwa Wakala umewekeza kwenye mashine za
kidigitali na wamewajengea uwezo wafanyakazi wake, ambapo kutokana na
uwezo huo wamefanikiwa kukidhi mahitaji ya wateja wake kwa wakati na kwa
ubora husika.
Aidha, Mkurugenzi
huyo ameeleza kuwa Wakala wamefanikiwa kutekeleza Mpango wao wa
biashara kwa kupata soko la uhakika la uchapaji hususani kwa Taasisi na
idara za serikali pamoja na sekta binafsi, hivyo wamefanikiwa kuongeza
mapato ya Serikali kupitia fedha zinazopatikana kupitia kazi za uchapaji
na ununuzi wa vifaa vya ofisi na kuandikia.
Tangu mwaka 2018,
Zanzibar imeanzisha rasmi Wakala wa Uchapaji wa Serikali Zanzibar,
chini ya Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale ambapo Wakala hiyo
imepewa uwezo kisheria wa kutoa huduma za uchapaji. Kwa upande wa
Tanzania Bara, Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa serikali ipo chini ya Ofisi
ya Waziri Mkuu ikiwa na jukumu la kutoa huduma ya uchapaji.
Idara ya Mpiga
Chapa Mkuu wa serikali imeabainisha lengo lake kuu kuwa, ni Kutoa
huduma za Uchapaji kwa wakati zenye ubora na kwa gharama nafuu. Idara
hiyo inaongozwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ambaye husimamia
vitengo vya Udhibiti wa Ubora, Uzalishaji, Ufundi, Masoko na Maduka ya
Vitabu ya Serikali.
No comments:
Post a Comment