Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza katika Kikoa
cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, wakati
alipofika Wilayani humo kwa ziara ya kikazi. Simbachawene amepiga
marufuku ukamataji wa wananchi, bodaboda pamoja na kufanya operesheni ya
aina yoyote kwa kukurupuka bila kufuata utaratibu, hali inayoweza
kusababisha uvunjifu wa amani badala ya kujenga amani.. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza katika Kikoa
cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mpwapwa, wakati alipofika
Wilayani humo kwa ziara ya kikazi. Simbachawene amepiga marufuku
ukamataji wa wananchi, bodaboda pamoja na kufanya operesheni ya aina
yoyote kwa kukurupuka bila kufuata utaratibu, hali inayoweza kusababisha
uvunjifu wa amani badala ya kujenga amani. Watatu kulia ni Mkuu wa
Wilaya hiyo, Jabir Shekimweri. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akisalimiana na Katibu
Tawala Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Ngalangasi, wakati
alipokuwa anawasili ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kukutana na Kamati ya
Ulinzi na Usalama, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (kushoto), akisalimiana na Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mpwapwa, Paul Sweya, wakati alipokuwa anawasili katika
Kikao cha Baraza la Madiwani Wilayani humo, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (kushoto), akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya
Mpwapwa, Jabir Shekimweri, wakati alipokuwa anawasili ofisini kwa Mkuu
wa Wilaya huyo kukutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (katikati), akimsikiliza Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Mpwapwa, Maulidi Manu, wakati alipokuwa akifafanulia jambo katika Kikao
cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, baada ya kuulizwa swali
na Waziri Simbachawene ambaye alifanya ziara ya kikazi wilayani humo,
leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
*******************************
Na Mwandishi Wetu, MOHA, Mpwapwa.
WAZIRI wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amepiga marufuku ukamataji wa
wananchi, bodaboda pamoja na kufanya operesheni ya aina yoyote kwa
kukurupuka bila
kufuata utaratibu, hali inayoweza kusababisha uvunjifu
wa amani badala ya kujenga amani.
Pia Waziri huyo
aliagiza kuwa, kila operesheni itakayopangwa kufanywa na Polisi Nchini,
wanapaswa watoe taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ili ajue nini kitafanyika kwa
kuwa yeye ni Mwenyikiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo,
na pia ndio utaratibu unapaswa kuwa hivyo.
Akizungumza
katika Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Wilaya ya Mpwapwa,
Mkoani Dodoma na baadaye kulisisitiza agizo hilo katika Kikao cha Baraza
la Madiwani Halmashauri ya Wilaya, leo, Simbachawene alisema ukamataji
usio na mpangilio hauna tija na unaweza kuvunja amani badala ya kujenga
amani.
“Wananchi
wanawalalamikia askari wetu sana kukamata bodaboda bila sababu, sio
bodaboda tu hata kukamata kamata hovyo watu, ukamataji mwingine unakua
kama kukomoana, hauna tija, hauleti amani, badala yake unasababisha
amani itoweke,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa,
“Yaani msako fulani unatungwa hauna kichwa wala mguu, hauna maelekezo
yoyote ya Mkuu wa Jeshi la Polisi au chombo, ni watu tu wanajitungia
wanaondoka na pikipiki yao wamepakiana wanaenda kufanya operesheni
ambayo haina utaratibu.”
Alisema vyombo
vya ulinzi na usalama ni vya wananchi, na operesheni yoyote haipaswi
kufanyika bila Mkuu wa Wilaya kupewa taarifa ambapo ndio utaratibu
unapaswa kuwa hivyo.
Pia Waziri
Simbachawene aliupongeza uongozi wa Wilaya hiyo kwa kuwa karibu na
wananchi kwa kusikiliza kero zao na kuifanya Wilaya hiyo kuendelea kuwa
na amani na utulivu na wananchi kuendelea kuwa na imani na viongozi hao.
“Endeleeni kuwa
karibu na wananchi, kwa kusikiliza kero zao na pia kuzitatua, na epukeni
malalamiko ya hapa na pale yasiyokuwa ya lazima,” alisema Simbachawene.
Aidha,
Simbachawene aliewaomba viongozi wa Wilaya hiyo kujipanga vizuri katika
maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka
huu.
“Mwaka huu ni wa
uchaguzi, wananchi kupitia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na taasisi
zote za utawala, mnapaswa kuwa na ushirikiano mkubwa ili kujenga msingi
wa uchaguzi utakaokuwa wa amani na utulivu,” alisema Simbachawene.
Alisema mwaka wa
uchaguzi haupaswi kuwa na vurugu, ni mwaka ambao unapaswa kuwa na
utulivu kwasababu ni jambo zuri la kidemokrasia linafanyika.
“Rai yangu kwa
wananchi, kuhakikisha kwamba tunapaswa kujenga utulivu kuanzia sasa
kuelekea uchaguzi mkuu, hatupaswi kuwa na vurugu, ni mwaka ambao amani
na utulivu wa nchi unajengwa kuanzia sasa, mshikamano wa vyombo vyetu
ndio msingi wa kujenga uchaguzi utakao kuwa wa huru na haki ambao
utafanya mwaka huu,” alisema Simbachawene.
Kwa upande wake,
Mkuu wa Wilaya hiyo, Jabir Shekimweri alimshukuru Waziri huyo na kuahidi
kuyafanyia kazi maelekezo yake aliyoyatoa katika kikao cha Kamati ya
Ulinzi na Usalama pamoja na Kikao cha Baraza la Madiwani.
Naye Mkuu wa
Polisi wa Wilaya ya Mpwapwa (OCD), ASP Maulidi Manu alisema ujio wa
Waziri huyo umewasaidia zaidi kwa kujipanga zaidi, na kufuata maagizo
yote aliyoyatoa kwa Jeshi la Polisi Wilayani humo.
“Tumefarijika kwa ujio wa Mheshimiwa Waziri, maagizo yake aliyoyatoa tunaahidi kuyafanyia kazi,” alisema Manu.
Waziri
Simbachawene, alifanya ziara ya siku moja kwa ajili ya kukutana na
Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Baraza la Madiwani Wilayani humo.
No comments:
Post a Comment