Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wajumbe wa kamati ya Maandalizi ya
Mkutano wa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa Sekta ya Kazi na Ajira wa Nchi
Wanachama wa SADC utakaofanyika tarehe 2 hadi 6 Machi, 2020 katika Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Sehemu ya wajumbe wa kamati ya
Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa Sekta ya Kazi na
Ajira wa Nchi Wanachama wa SADC wakifuatilia maelekezo ya Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani).
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya
Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa Sekta ya Kazi na
Ajira wa Nchi Wanachama wa SADC wakifuatilia maelekezo ya Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani).
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Tanzania inatakuwa mwenyeji wa
Mkutano wa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa Sekta ya
Ajira na Kazi kutoka
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
unaotarajiwa kufanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 2 hadi 6
Machi 2020.
Mkutano huu ambao utafunguliwa
na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan, umebeba kaulimbiu isemayo “Kukuza Soko la Ajira na Mahusiano Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu”.
Akizungumza na Kamati ya
Maandalizi ya Mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu
wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, Serikali ya Tanzania
imejipanga vizuri kuwapokea Mawaziri 15 kutoka Nchi za SADC na kuwataka
wajumbe wa Kamati hizo kukamilisha maandalizi kwa kuzingatia viwango
ambavyo tayari vimewekwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa
Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika mwaka 2019 hapa nchini.
“Tanzania ni Mwenyekiti wa
SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja. Tumeendelea kuwa na Mikutano kadhaa ya
kisekta tangu ulipofanyika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali
wa SADC mwaka 2019. Nawahimiza tuendelee kuandaa mikutano hii kwa
kufuata viwango vya juu vilivyowekwa na Mhe. Rais wetu wakati wa Mkutano
huo na mingine iliyofuata hadi hapo tutakapokabidhi uenyekiti kwa nchi
nyingine” alisisitiza Mhe. Mhagama.
Aidha, Mhe. Mhagama alipokea
taarifa za utekelezaji wa majukumu ya kamati ndogo ndogo ikiwa ni pamoja
na kupitia ratiba ya Mkutano ambapo mbali na kushiriki Mkutano huo,
Mawaziri hao watapata fursa ya kufanya ziara katika maeneo kadhaa
ikiwemo Chuo Don Bosco Net Tanzania kilichopo Dar es Salaam kwa
ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana wanaosoma
chuoni hapo. Pia Mawaziri watatembelea maoneo mbalimbali ya kihistoria
yaliyopo Bagamoyo lengo ikiwa ni kutangaza vivutio vya utalii vya
Tanzania.
Kadhalika, Mawaziri hao
watashuhudia uzinduzi wa Programu ya Taifa ya Mafunzo kwa Vitendo mahala
pa kazi kwa vijana (Internship) utakaofanyika tarehe 5 Machi 2020
sambamba na ufunguzi rasmi wa Mkutano huo. Mkutano huu ni mwendelezo wa
mikutano ya kisekta ya SADC ambayo itafanyika nchini kwa kipindi cha
mwaka mmoja, kufuatia Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo hadi
mwezi Agosti 2020.
Mkutano wa Mawaziri ambao
utatanguliwa na vikao vya maandalizi vya Makatibu Wakuu na Wataalam
vitakavyofanyika kuanzia tarehe 2 Machi 2020, unatarajiwa kuhudhuriwa na
washiriki kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ikiwemo Tanzania.
No comments:
Post a Comment