Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo pamoja na mkewe Veronica Wangabo wakiwasalimia watoto
waliohudhuria ibada ya kuukaribisha mwaka 2020 katika Kanisa Katoliki
Parokia ya Kristu Mfalme Sumbawanga mjni.
*******************************
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amesema ili kukabiliana na ukatili dhidi ya
watoto, serikali
haina budi kufanya kazi kwa karibu na viongozi wote wa dini wa madhehebu
mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo kuwataka kuwa karibu na watoto ili
watoto hao wawe huru kuwataarifu viongozi hao aina yoyote ya manyanyaso
wanayoyapata wakiwa nyumbani.
Amesema kuwa kwa muda mrefu katika
mkoa watoto wamekuwa wakiathirika kutokana na ugomvi baina ya wazazi na
hatimae kutopata mapenzi ya baba na mama hali inayopelekea watoto hao
kutopata malezi mazuri ya kifamilia na hatimae kuishia mitaani na kuwa
na kizazi kisichofaa katika jamii na kusisitiza kuwa serikali ya mkoa
imejizatiti kupambana na hali hiyo.
“ Chimbuko la maisha yetu wote
liko kwenye familia na familia ni watoto, kwahiyo tujielekeze zaidi
katika malezi ya watoto wetu, lakini pia kuhakikisha ya kwamba tunawapa
na kuheshimu haki zao, haki za watoto tunakwenda kuzifungua kwa watoto
wetu wote kama serikali, tutawaelimisha watoto haki zao, tutawaambi
wakifanyiwa manyanyaso waende kwa nani, waripoti kwa nani matatizo
hayo,” Alisema
“lakini narudi kwa viongozi wa
dini na wenyewe tutawaomba wawe karibu sana na watoto ili watoto waweze
kufunguka wawaambie manyanyaso wanayoyapata majumbani, nasi
tutashirikiana na viongozi wa dini kupambana na hayo manyanyaso na huo
ukatili wa watoto” Alisisita.
Mh. Wangabo ameyasema hayo
alipokuwa akitoa salamu zake za mwaka mpya katika ibada ya kuukaribisha
mwaka 2020 iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristu Mfalme,
mjini Sumbawanga.
Mwishoni mwa mwaka 2019 ofisi ya
mkuu wa mkoa wa Rukwa ulizindua mpango mkakati wa wa miaka mitano wa
kukabiliana na kupambana na mimba za watoto pamoja na kupunguza watoto
wa mitaani, mpango ambao utekelezaji wake unaanza mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment