
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma
leo kuhusu ajira kwa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga
Taifa “Operesheni
Magufuli” na masuala mbalimbali ya kiutumishi.
Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael.
Na.Alex Sonna,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameelekeza vijana wote wenye
elimu ya Shahada ya Kwanza waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) “Operesheni Magufuli” kupewa ajira katika taasisi mbalimbali za serikali.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake eneo
la Mtumba jijini Dodoma leo.
“Serikali imekuwa ikiwajengea
vijana uadilifu, umoja, mshikamano, moyo wa kujitolea, moyo wa uzalendo,
nidhamu na ari ya kupenda kufanya kazi kwa kuwaingiza kwenye mafunzo ya
Jeshi la Kujenda Taifa, hivyo kwa kutambua mchango wao, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza wapewe
ajira’’ Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Dkt. Ndumbaro ametaja sifa za
vijana waliohitimu JKT kuwa ni lazima wawe wametumikia kwa kipindi
kisichopungua miaka miwili na kwamba wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao
binafsi, vyeti vya elimu, taaluma na vyeti vya kuhitimu mafunzo ya JKT
katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
kupitia barua pepe ya ps@utumishi.go.tz.
Aidha, Dkt. Ndumbaro ametumia
fursa hiyo kuwaasa waajiri wanaowarejesha makazini watumishi wa umma
walioghushi vyeti vya elimu na taaluma kwa visingizio kwamba
waliondolewa kimakosa au waliajiriwa kabla ya tarehe 20 Mei, 2001 kwa
sifa ya Elimu ya Darasa la Saba.
“Serikali haitosita kumchukulia
hatua mwajiri yeyote atakayekiuka maelekezo halali yaliyotolewa na
Serikali kuhusiana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi
walioghushi vyeti” Dkt. Ndumbaro amesema.
Akizungumzia suala la udanganyifu
na upendeleo katika upandishwaji vyeo, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa ofisi
yake imebaini baadhi ya waajiri kuwasilisha taarifa za uongo Ofisi ya
Rais-Utumishi ili kuwapandisha vyeo watumishi kwa lengo la kuwanufaisha
baadhi yao bila kuwa na vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria na
Kanuni zinazosimamia Utumishi wa Umma.
“Ofisi yangu itaendelea
kuwachukulia hatua stahiki waajiri watakaobainika kufanya udanganyifu
kwa madhumuni ya kuipotosha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora ili iweze kutoa vibali vya kuwapandisha vyeo
watumishi isivyostahili” Dkt. Ndumbaro amefafanua.
Dkt. Ndumbaro amehitimisha mkutano
huo kwa kuwataka Maafisa Utumishi nchini kufanya kazi kwa weledi kwa
kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma badala ya kuwa
chanzo cha kero na matatizo ya kiutumishi.
Mkutano kati ya Katibu Mkuu, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro na
waandishi wa habari ulikuwa na lengo la kuuhabarisha umma juu ya masuala
mbalimbali ya kiutumishi.
No comments:
Post a Comment