
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya
limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani
ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa mkoa huu wanaendelea kuwa
salama na mali zao. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea
kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa usalama hali inayopelekea
kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa
ya uhalifu, ajali za barabarani na kukamatwa kwa watuhumiwa mbalimbali
wa uhalifu.
Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na misako na doria ni kama ifuatavyo:-
- KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kupatikana na Nyara za Serikali
vipande kumi na moja [11] vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilo 21.5
sawa na Tembo 4 wenye thamani ya Tshs 137,970,000/=. Watuhumiwa hao ni:-
- ABDULMARIK UPETE [41] mkazi wa Uyole
- MOHAMED OMARY [50] mkazi wa Kilosa Mkoani Morogoro na
- AYOUB KIDUMBA [49] mkazi wa Ilembula Mkoani Njombe.
- LAWI KALONGA [50] mkazi wa Mkoani Dodoma.

Watuhumiwa walikamatwa Disemba 21,
2019 majira ya saa 18:30 jioni huko eneo la Soweto lililopo Kata ya
Ruanda, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya baada ya Jeshi la Polisi kuweka
mtego. Nyara hizo zilisafirishwa kutoka Mkoani Njombe kwa lengo la
kutafuta wateja na zilikuwa zimehifadhiwa kwenye duka la kuuza vipuri
vya magari mali ya ABDULMARIK UPETE. Taratibu za kisheria zinafanywa ili
watuhumiwa wafikishwe Mahakamani.
- KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KULIPIA USHURU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linawashikilia watuhumiwa wawili [02] kwa tuhuma za kuingiza nchini
bidhaa aina ya vitenge belo 24 kila belo moja likiwa na doti 50 za
vitenge sawa na doti 1,200 kutoka nchini Zambia bila kulipia ushuru.
Mzigo huo ulikuwa unasafirishwa kwenye gari T.471 BJJ aina ya Toyota
Hiace. Watuhumiwa waliokamatwa ni:-
1.ELIA MWAKAGILE [30] mkazi wa Mwakibete na
2.FURAHA LUTENGANO MWAKALENGELA [35] mkazi wa Mwakibete.

Watuhumiwa wamekamatwa Disemba 22,
2019 majira ya saa 03:00 usiku huko eneo la Ituta lililopo Kata na
Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya – Tunduma.
Taratibu zinafanywa ili watuhumiwa pamoja na mzigo huo kukabidhiwa Mamlaka ya Mapato [TRA] kwa hatua za kiforodha.
iii. KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KULIPIA USHURU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linamshikilia mtuhumiwa mmoja [01] MARIAM JAPHET [35] Mkazi wa Ilembo –
Mbeya kwa tuhuma za kuingiza nchini bidhaa aina ya vitenge doti 42
kutoka nchini Malawi bila kulipia ushuru.

Mtuhumiwa amekamatwa Disemba 22,
2019 majira ya saa 06:30 alfajiri huko eneo la stendi ya mabasi Kyela,
iliyopo Kata ya Kyela – Kati, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa
wa Mbeya.
Taratibu zinafanywa ili mtuhumiwa pamoja na mzigo huo kukabidhiwa Mamlaka ya Mapato [TRA] kwa hatua za kiforodha.
- KUKAMATWA WATUHUMIWA WANAOJIHUSISHA NA
MTANDAO WA WIZI WA PIKIPIKI NA MATUKIO MENGINE
YA UHALIFU.
Katika kipindi hiki cha kuelekea
mwishoni mwa mwaka – 2019 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya msako
maeneo mbalimbali Mkoani Mbeya dhidi ya wahalifu wa matukio mbalimbali
ikiwemo mtandao wa wizi wa Pikipiki.
Katika misako iliyofanyika
jumla ya watuhumiwa wanne [04] wamekamatwa, wamehojiwa na
wamekiri
kufanya matukio kadhaa ya uporaji wa Pikipiki na kuziuza nchi jirani ya
Malawi na Zambia.
Watuhumiwa waliokamatwa katika misako ya hivi karibuni ni pamoja:-
- ADAM BRAYSON SANGA [27] Bodaboda, mkazi wa Iyunga
- OSCAR ELIAS MWAKABIKI [25] mkazi wa Utengule – Mbalizi na
- BENJAMIN SILVESTER MWANDATA [26] Bodaboda na mkazi wa Utengule – Mbalizi.
4: RAMADHAN BAKARI [25] mkazi wa Lupa – Chunya.
- KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA WIZI KWENYE MAGARI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
litaendelea kufanya misako na doria katika maeneo yote ili kuhakikisha
linasambaratisha mtandao wa wizi wa Pikipiki na wahalifu wengine kwa
kushirikiana na wananchi na wadau wengine vikiwemo vyombo vya ulinzi na
usalama ndani ya Mkoa wa Mbeya.
Kutokana na kuibuka kwa wizi
wa vifaa vya magari katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya, Jeshi la
Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya misako na kufanikiwa kuwakamata
watuhumiwa wanne [04] kuhusiana na matukio ya wizi kwenye magari,
kuvunja vioo vya magari na kuiba betri za magari, kufungua milango ya
magari na kuiba vitu vya thamani.
Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na matukio hayo ni:-
- JOSEPH SIMON @ MBOGOLO @ WHITE [40] Mkazi wa Mwananyamala D’Salaam.
- FAIDHA NSAJIGWA @ MWASEBA [44] Mkazi wa Isanga.
- GABRIEL MWANDWANGA [48] Mkazi wa Manga – VETA.
- AYOUB EMANUEL KISUNGA [22] Mkazi wa Iyela
Watuhumiwa hao walikutwa na vifaa
vya kuvunjia magari na baada ya kuhojiwa wamekiri kuhusika na matukio
kadhaa ya wizi kwenye magari katika maeneo ya Forest, Kabwe, Isanga,
Uyole, Sokomatola na Mwanjelwa Jijini Mbeya. Pia wamekiri kufanya
matukio kama hao katika mikoa ya Arusha na Tanga.
Misako na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu Mkoani Mbeya inaendelea vizuri.
- MAUAJI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linawashikilia watu wawili mke na mume ambao ni ALLY MBAVU [23] na
SABINA ALEX [19], wakazi wa Pambogo kufuatia kifo cha mtoto wao ISMAIL
ALLY MBAVU [mwaka 1 na miezi 11]
Tukio hilo limetokea Disemba
22, 2019 majira ya saa 06:30 alfajiri huko mtaa wa Pambogo, Kata ya
Iyela, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya. Marehemu alitoweka nyumbani kwao
tangu Disemba 21, 2019 jioni na hakuonekana mpaka alipokutwa amefariki
dunia.
Uchunguzi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika, watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.
vii. KUELEKEA SIKUKUU ZA KRISMAS NA MWAKA MPYA.
Katika kuelekea sikukuu za
Mwisho wa Mwaka [Krismas] na Mwanzo wa Mwaka [Mwaka Mpya] Jeshi la
Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kikamilifu kuhakikisha wakazi wa Mkoa
wa Mbeya, wageni na wakazi wa mikoa jirani wanasherehekea sikukuu hizo
kwa amani na utulivu.
Kwa kutambua kuwa Mkoa wetu
unapakana na nchi jirani ya Malawi pia barabara kuu inayounganisha nchi
yetu na nchi jirani pamoja na mikoa jirani imepita hapa, tumejipanga
vizuri kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara wakiwemo madereva
na watembea kwa miguu. Wito wangu kwa watumiaji wote wa barabara
kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka
ajali zinazoweza kuepukika.
Kuelekea kipindi hiki cha
sikukuu, waumini wa madhehebu mbalimbali ushiriki katika ibada/misa kwa
nyakati tofauti kulingana na ratiba zao, Jeshi la Polisi limejipanga
kuhakikisha ulinzi na usalama katika makanisa pamoja na misikiti hasa
katika misa au ibada za mkesha. Aidha ninatoa wito kwa viongozi katika
makanisa na misikiti kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri hasa katika
suala la ulinzi kwa kuunda kamati za ulinzi na usalama ili kuhakikisha
ulinzi unakuwepo maeneo ya ndani na nje ya Makanisa na Misikiti.
Pia rai kwa wamiliki wa Kumbi
za starehe kufuata sheria hasa kuzingatia Leseni zao za biashara
zinavyowaelekeza ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wa kufungua na
kufunga sehemu zao za biashara, wenye kumbi za muziki kuhakikisha kambi
zao zinaingiza idadi ya watu inayohitajika [capacity] pamoja na kuweka
walinzi katika maeneo yanayowazunguka.
Kuelekea msimu huu wa sikukuu,
ni wito wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa wazazi, walezi na jamii
kwa ujumla kuzingatia ulinzi wa mtoto, na pia kuwasaidia watoto hasa
kuwavusha katika maeneo tete kama vile barabarani au maeneo yenye mito
ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata. Pia ili kuepuka watoto kupotea
katika kipindi cha sikukuu, wazazi na walezi wanapaswa kuongeza umakini,
uangalizi wa watoto wao kila mahali wanapokwenda iwe ni makanisani,
misikitini au katika maeneo yenye michezo ya watoto ikiwemo fukwe za
ziwa nyasa Matema na Ngonga Wilayani Kyela.
Mwisho, nitumie fursa hii kuwatakia wananchi wote wa mkoa wa Mbeya na Watanzania kwa ujumla Kheri ya Krismas na Mwaka Mpya 2020 tukumbuke kufanya vitu kwa kiasi, tusivuke viwango/mipaka.
No comments:
Post a Comment