Mfanya
Biashara wa Bidhaa ya Mchele ulioangamizwa tani 105 kutoka Kampuni ya
Ahmed Khelef, Ibrahim Omar Awesu akitoa maelezo kuhusu kuharibika kwa
bidhaa hiyo huko Jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.
Mkuu wa Kitengo cha Uchambuzi wa athari zitokanazo na Chakula kutoka Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) Aisha Suleiman akitoa maelezo kuhusu bidhaa mbali mbali za Chakula tani 133.5 zilizoharibika na kuangamizwa huko Jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.
Wafanyakazi kutoka Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) wakiangamiza bidhaa mbali mbali za Chakula na Vipodozi katika Jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.
Picha na Maryam Kidiko – Habari Maelezo Zanzibar.
******************************
Na Miza Kona Maelezo Zanzibar 02/11/2019
Wakala wa
Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) imeteketeza zaidi ya tani 130
za
bidhaa za chakula na tani tano za vipodozi zilizoharibika katika jaa
la Kibele wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumza na
waandishi wa habari Mkuu wa Kitengo cha uchambuzi wa Athari zitokanazo
na Chakula wa ZFDA Aisha Suleiman amesema bidhaa hizo zilikaguliwa na
kuonekana hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Alisema kuwa
bidhaa hizo ambazo baadhi yake zikiwa zimeharibika na nyengine zikiwa
zimeingia nchini bila kufuata utaratibu wa uingizaji bidhaa zilikamatwa
katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Alizitaja bidhaa
zilizoangamizwa kuwa ni mchele tani 105 ulioingizwa na kampuni ya Ahmed
Khelef, majani ya chai tani 24 kutoka kampuni ZATEPA, bidhaa
mchanganyiko tani moja, pipi tani moja na nusu kutoka kampuni Basil Cook
pamoja na soda za kopo tani mbili kutoka kampuni ya Ahmed Salim.
Amefahamisha
bidhaa zinazoingia nchini zinatakiwa kufuata taratibu zote za uingizaji
ikiwa pamoja na kufanyiwa ukaguzi na maafisa wa Wakala wa Chakula na
Dawa ili kuhakikisha kuwa bidhaa hizo zipo salama na hazina madhara kwa
mtumiaji.
Aidha Mkuu huyo
amewataka wafanya biashara na wananchi kuwa waangalifu wakati wanapnunua
na kusafirisha bidhaa ili kuhakikisha zinaingia nchini zikiwa bado
hazijaharibika.
Kaimu Mkurugenzi
Idara ya Dawa na Vipodozi wa ZFDA Nassir Buheti amesema vipodozi
vilivyotekezwa baadhi yake vina sumu ambayo ni hatari kwa afya ya
binadamu.
Amefahamisha kuwa
vipodozi hivyo vimeingia nchini kinyume na utaratibu havijaisha muda
wake wa matumizi bali vimeonekana kuwa vinaviambato vyenye sumu havipo
salama kwa mtumiaji.
Kwa upande wake
Mfanyabiashara Ibrahim Omar Awesu kutoka Kampuni ya Ahmed Khelef alisema
walinunua mchele huo ukiwa katika hali nzuri kwa matumizi lakini
uliharibika kutokana na kampuni ya usafirishaji kuchelewa kuusafirisha
na kusababisha na hatimae kuharibika ukiwa njiani kuja Zanzibar.
Aidha ameomba
wakala wa Chakula wa Dawa kufanya mapema ukaguzi wa bidhaa zinazoingia
nchini pamoja na makampuni ya usafirishaji kuingiza bidhaa hizo kwa
wakati ili kuepuka hasara.
No comments:
Post a Comment