Mgeni rasmi wa mahafali ya
17 ya Taasisi ya uhasibu Tanzania (TIA) kwa kampasi za Singida, Mwanza
na Kigoma, Dkt. Rehema Nchimbi akihutubia kwenye mahafali hayo
yaliyofanyika mkoani Singida jana.
Mratibu wa Taaluma Kampasi ya Singida, Abbas Sanga akizungumza kwenye mahafali hayo.
Mhitimu bora wa Shahada ya
Uongozi wa Rasilimali Watu kutoka Kampasi ya Singida Emmanuel Matikiti
akipokea zawadi kutoka kwa mgeni rasmi Dkt. Rehema Nchimbi.
Wahitimu wa kozi ya Astashahada ya Uhasibu muda mfupi kabla ya kutunukiwa.
Mhitimu wa Shahada ya
Uhasibu kutoka kampasi ya Singida Livingstone Ruzikamunzira akipokea
cheti kutoka kwa mgeni rasmi Dkt. Rehema Nchimbi kwenye mahafali hayo.
Wahitimu wa kozi ya Shahada ya Uhasibu wakiwa mbele ya mgeni rasmi kabla ya kuanza zoezi la kuwatunuku
Mgeni rasmi Dkt. Rehema
Nchimbi (waliokaa katikati) akiwa na Wahitimu wa kozi mbalimbali kwenye
mahafali ya 17 ya TIA mkoani Singida.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KWA mara ya kwanza tangu
kuanzishwa kwa Kampasi za Singida na Mwanza chini ya Taasisi mahiri na
kongwe ya uhasibu nchini (TIA) hapakuwepo na kozi ya Shahada ndani ya
kampasi zake za Singida na Mwanza. Hivyo wahitimu wa kozi ya shahada kwa
mwaka wa masomo 2018/2019 ndio wanaofanikiwa kuandika historia ya
kuhitimu kozi hiyo kwa mara ya kwanza.
Katika mahafali ya 17 ya
(TIA) kwa Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma, na mahafali ya nane kwa
kampasi ya Singida, jumla ya wahitimu 209 wamehitimu kozi ya Shahada,
huku wengine 328 wakihitimu kozi ya Stashahada, Astashahada 504 na ngazi
ya cheti 647 wote wakihitimu katika kozi za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi,
Uongozi wa Rasilimali Watu na Usimamizi wa Biashara.
Akizungumza kwenye mahafali
hayo, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango mkoani hapa jana,
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, mbali ya kupongeza juhudi
lukuki zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuboresha ubora wa taaluma
na wanataaluma, aliwasihi wahitimu hususan wale wa shahada na uongozi
mzima wa TIA kuanza kutumia sifa na ubora wa kitaaluma walionao katika
kuongeza thamani kwa wananchi walio mitaani hususan vijana.
Dkt Nchimbi aliwatakafarisha
na kuwataka wahitimu kujiuliza je sura ya kampasi hiyo huko nje ikoje?
Kampasi hii inavyosifika kwa ubora je na akina mama lishe na waendesha
bodaboda wanaoizunguka na kuihudumia kila kukicha nao wamepata fursa ya
kuambukizwa ubora huo? Je kampasi hizi zinaonekanaje huko nje katika
kubadili na kuongeza thamani hususan kwa vijana ili kuchagiza na kuleta
chachu ya mabadiliko ya fikra kufikia maendeleo stahiki na ya
kiushindani
“Je haiwezekani TIA kuwa na
mafunzo ya muda mfupi kwa vijana wetu, waendesha bodaboda, mama lishe na
wajasiriamali angalau na wao wakawa na mahafali yao ya kila wiki
itapendeza, na itaongeza ubunifu tija na ufanisi ndani na nje ya kampasi
zetu kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema Dkt Nchimbi
Alisema watumishi wa Singida
wamejiwekea kauli mbiu yao inayojulikana kama “ Mshahara wangu uko
wapi”? huku akichekesha wahitimu kuwa kuna watumishi ambao wameshapokea
mshahara wa mwezi Novemba mwaka huu, lakini ukimuuliza mpaka sasa hauoni
Zaidi ya kulalamika mshahara hautoshi! Na kutoa rai kwa wanajumuiya ya
TIA kuangalia namna ya kuanzisha somo mahususi la “mshahara hautoshi,”
akiamini ni taasisi hiyo pekee na wahitimu wake ndio jawabu la kutamka
kwanini hautoshi, uko wapi na kutupa maarifa na stadi stahiki za siku
zote kuiona mishahara yetu.
Aidha, akizungumzia kuhusu
ubora wa elimu ndani ya taasisi Dkt Nchimbi alisema fani zinazotolewa na
TIA ni muhimu sana katika kuendesha uchumi wa taifa, hususan katika
kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma, hivyo aliwataka kuzidisha
kasi ya umahiri huo katika kufanikisha azma ya sera iliyopo ya Tanzania
ya Viwanda.
Alisema dunia ya sasa
imetamalaki teknolojia na utandawazi hivyo jukumu lililopo ni kuendelea
kuboresha mitaala ndani ya taasisi ili wakati wote ikidhi viwango vya
kimataifa, hususan umahiri badala ya maarifa. Na kuwasihi kuzidisha
kuzalisha wataalamu wenye weledi, maarifa na umahiri wa kutatua
changamoto na sio kuziongeza.
“Zingatieni kwa umakini
suala la umahiri katika mitaala yenu ili tuweze kuwa na wataalamu wenye
uwezo wa kulifikisha taifa kwenye uchumi wa kipato cha kati kabla ya
ishirini ishirini na tano (2025),” alisema Dkt Nchimbi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wakili Said Musendo
Chiguma, alisema jukumu la bodi ya ushauri, pamoja na mambo mengine ni
kutoa ushauri kwa TIA kwa nia ya kutekeleza na kuendeleza jitihada za
serikali kulingana na malengo makuu yaliyoianzisha.
Chiguma alisema lengo hasa
la taasisi hiyo ni kutayarisha wahitimu kwa uboreshaji endelevu wa
mitaala, azma ikiwa ni kuandaa wafanyakazi wenye weledi na uwezo wa
kujiajiri, sambamba na maboresho hayo kuzingatia juhudi za kujenga
uzalendo, uaminifu na maadili, huku akisisistiza kwamba mhitimu asiye na
sifa hizo siyo rasilimali kwa taifa.
Alisema kwa matokeo ya
vigezo hivyo taasisi imeendelea kupendwa na kuwa kivutio kikubwa, hali
iliyopelekea ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi kila mwaka licha ya
kuwepo vyuo vingi vya ushindani idadi inayofikia jumla ya wanafunzi
18,585 katika kampasi zake zote sita ambazo zimesambaa kimkakati.
“TIA ni taasisi ya serikali,
imeweza pia kuchangia bilioni mbili na milioni mia tano (2,500,000,000)
kama ziada ya mapato yake serikalini,” alisema Wakili Chiguma.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu
wa TIA, Luciana Hembe, alisema Taasisi hiyo kwa sasa ina kampasi 6
zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam (Makao Makuu), Mbeya, Singida,
Mtwara, Mwanza na Kigoma, zote zikiwa na jumla ya wanachuo 18, 587, huku
jumla ya kozi zinazotolewa katika kampasi zote ni 20.
Hembe alibainisha kuwa, kwa
mwaka 2019 katika kampasi zote kuna jumla ya wahitimu 8695 ikiwa ni
ongezeko la asilimia 35.5 ikilinganishwa na wahitimu 6418 kwa mwaka
2018. Alisema mahafali hayo ni kwa wahitimu wa TIA ngazi tofauti Kampasi
za Singida, Mwanza na Kigoma kwa mwaka wa masomo 2018/2019.
Alisema idadi ya wahitimu
wote waliohudhuria na wasiohudhuria mahafali hayo katika kozi ya Cheti
cha Awali, Astashahada na Shahada ni 1,688 wakiwemo wanawake 915 sawa na
asilimia 54.21, na wanaume 773 sawa na asilimia 45.79
No comments:
Post a Comment