Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof Charles Majinge akikata utepe
kuashiria kuzinduliwa kwa ICU mbili za watoto wanaohitaji uangalizi
maalumu PICU na NICU. Kulia ni Mwakilishi wa Malkia wa Sharja, Dkt.
Sawsan Abdul Salam Al Madhi akishiriki katika uzinduzi na Mwenyekiti wa
Bodi ya Tumaini la Maisha (TLM), Bw. Gerald Mongella akishuhudia tukio
hilo. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa MNH, Dkt. Ellen Senkoro
naye akishudia tukio hilo leo. Mke wa Mfalme wa UAE, Shaikha Jawaher
Bint Mohammed AlQasim amefadhili ujenzi wa wodi mbili za watoto chini ya
siku 28 na kuanzia umri wa mwaka mmoja kuendelea kwa thamani ya
shilingi bilioni 4.9.
Mojawapo ya ICU ya watoto wenye umri wa siku 29 hadi miaka 14 iliyozinduliwa leo.
Mwakilishi wa Malkia wa Sharja,
Dkt. Sawsan Abdul Salam Al Madhi akizungumza katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) kabla ya kuzinduliwa kwa ICU mbili za watoto wanaohitaji
uangalizi maalumu ya PICU na NICU. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya
Wadhamini wa MNH, Dkt. Ellen Senkoro.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
wa MNH, Prof. Charles Majinge akizungumza na wataalamu wa afya kabla ya
uzinduzi wa wodi hizo. Kulia ni Mwakilishi wa Malkia wa Sharja, Dkt.
Sawsan Abdul Salam Al Madhi na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa MNH, Dkt.
Hedwiga Swai wakimsikiliza Prof. Majinge.
……………….
Tanzania ni nchi mojawapo duniani
iliyofanikiwa kupunguza idadi ya vifo vya watoto walio
chini ya miaka
mitano kwa theluthi mbili na imesababisha kufikia mpango namba nne wa
malengo ya millennia.
Mafanikio haya yamekuja baada
ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Tumaini la
Maisha (TLM) kujenga ICU mbili za watoto wanaohitaji huduma za uangalizi
maalumu. Kutokana na juhudi hizo, Muhimbili imefanikiwa kupunguza vifo
vya watoto waliokuwa wanahitaji uangalizi maalumu kutoka asilimia 70 ya
vifo vilivyokuwa vikitokea ndani ya saa 24 na kufikia asilimia 30.
Hayo yamesemwa leo na
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa MNH, Dkt. Hedwiga Swai kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru wakati wa uzinduzi wa
ICU zinazowahudumia watoto wanaohitaji uangalizi maalumu chini ya umri
wa siku 28 (Neonatal Intensive Care Unit) na watoto wenye umri wa kati
ya mwezi mmoja hadi miaka 9 (Pediatric Intensive Care Unit) zenye
dhamani ya shilingi bilioni 4.9 zilizojengwa kwa ufadhili wa Mke wa
Mfalme wa UAE, Shaikha Jawaher Bint Mohammed AlQasim kupitia Shirika la
Tumaini la Maisha (TLM).
“Hospitali ya Taifa Muhimbili
ndiyo Hospitali kubwa kuliko hospitali zote nchini, idara ya watoto
wenye umri siku 0 mpaka 28 kina vitanda (baby cots) 134 na umri wa siku
29 mpaka miaka 14 kina vitanda 294 na ndicho kitengo chenye vitanda
vingi nchini. Kitengo hiki kinahudumia watoto wote wanaozaliwa Muhimbili
na wanaoletwa kwa njia ya rufaa kutoka takribani hospitali zote za
mikoa nchini,” amesema Prof. Museru.
Dkt. Swai amesema kwa kipindi
kirefu watoto walikua hawana ICU maalumu kwa ajili yao hivyo kulazwa
ICU ya kawaida ya watu wazima hali iliyosababisha watoto hao kukosa
huduma muhimu.
“Uwepo wa ICU hizi maalumu kwa
watoto utafanya watoto waweze kuonwa kwa ukaribu na madaktari na wauguzi
waliobobea katika kutoa huduma stahiki kwa watoto tofauti na awali
ambapo watoto walichanganywa kwenye ICU za watu wazima,” amesema Dkt.
Swai.
Pia, amesema katika kuendelea
kutekeleza maazimio ya mpango namba nne wa milenia wa kupunguza vifo vya
watoto chini ya miaka mitano, Muhimbili imefanikiwa kuwa na muongozo
wake wa kutoa huduma kwa watoto wachanga na watoto chini ya miaka 14
(PICU Guidelines).
“Haya ni mafanikio makubwa
sana kwani tumefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka
asilimia 19.2 mwaka 2017/2018 mpaka asilimia 16.2 mwaka 2018/2019. Haya
ni mafanikio makubwa kwetu katika kipindi cha mwaka mmoja,” amesema Dkt.
Swai.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Charles Majinge ameshukuru
Shirika la Tumaini la Maisha (TLM) na malkia wa Sharja kwa msaada huo,
pia ameutaka uongozi wa Muhimbili kuhakikisha hizi ICU zinatunzwa ili
watoto wote watakaopitia hapo waweze kunufaika na huduma za uangalizi
maalumu.
No comments:
Post a Comment