************************************
“Taasisi za fedha zaahidi kuongeza kasi ya malipo kwa wakulima ambao bado hawajalipwa”
Shinyanga,
Naibu Waziri wa Kilimo ndugu
Hussein Bashe amefanya kikao na wadau zao la pamba kujadili
changamoto
zinazolikabili zao hilo. Kikao hicho kilichofanyika mkoani Shinyanga
katika ofisi za Bodi ya Pamba kiliwahusisha wanunuzi wakubwa wa pamba,
taasisi za kifedha na wakuu mikoa, wilaya zinazolima pamba nchini.
Kikao hiki kimefanyika kufuatia
malalamiko ya baadhi ya wakulima kucheleweshewa malipo ya fedha zao za
msimu uliopta pia kukiwa na uhaba wa mbegu za pamba kwa wakulima wakati
msimu wa kupanda ukiwa unaelekea ukingoni.
Akiongoza kikao hicho ndugu Bashe
alisisitiza umuhimu wa wanunuzi wa pamba na taasisi za kifedha kufanya
kazi kwa ukaribu ili kuhakikisha malipo yanafanyika mara moja kwa
wakulima, ambapo baada ya majadiliano ya muda mrefu ilikubaliwa malipo
yote yawe yamefanyika kufikia Disemba 8.
Pia wasambazaji wakuu wa mbegu kwa
pamoja wamekubaliana kushirikiana kuhakikisha wakulima wanakopeshwa
mbegu bora upesi katika maeneo wanayohudumia kwa kutumia mfumo wa
wasambazaji hao kubadilishana mbegu ili kupunguza muda unaotumika
kusafirisha mbegu hizo.
Wakuu wa mikoa na wilaya
waliohudhuria kikao hicho walielezea wasiwasi wao juu ya baadhi ya vyama
vya ushirika (AMCOS) kutowalipa wakulima, pamoja na kwamba vimekwisha
lipwa fedha ambapo iliamuliwa vyama hivyo na wakulima wafungue akaunti
katika mabenki ili utaratibu wa malipo kuanzia msimu ujao ufanyike kwa
njia ya benki chini ya usimamizi wa wakuu wa wilaya.
Nao wawakilishi wa taasisi za
kifedha walielezea namna walivyojipanga kuhakikisha malipo ya wakulima
yanalipwa kupitia benki kwa kuhakikisha kila mkulima anafungua akaunti
katika benki zao. Taasisi zilizohudhuria ilikuwa benki za NMB, CRDB,
Azania, NBC na Benki ya Posta.
Naibu Waziri wa Kilimo Hussein
Bashe alitumia fursa hiyo kuwafahamisha wafanyabiashara juu ya tamko la
Rais John Pombe Magufuli kuwa Serikali haitoingilia kupanga bei ya mazao
ya wakulima na badala yake itabaki kuwa msimamizi wa kuhakikisha
mkulima anapata haki yake, ambapo aliwapa onyo wafanyabiashara kutotumia
mwanya huo kujaribu kuwanyonya wakulima.
No comments:
Post a Comment