Waziri wa Katiba na Sheria
Mheshimiwa Balozi Dkt Augustine Mahiga amewataka Wakuu wa Magereza
nchini kutumia nguvu kazi na ujuzi wa wafungwa walioko magerezani kubuni
miradi mbalimbal ili kuwazalishia fedha zitakazowawezesha kujiendesha
bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Balozi Mahiga ameyasema hayo leo
alipotembelea gereza la Kyela kujionea jinsi Taasisi za
Haki Jinai
zinavyotekeleza majukumu yake katika mahakama na magereza ikiwemo
kutatua changamoto ya mrundikano wa mahabusu katika magereza pamoja na
kuboresha mfumo wa utoaji haki na hali ya magereza kote nchini.
“Nguvu kazi za hawa wafungwa ni
nyingi na wana ujuzi mbalimbali mnaoweza kuutumia kuanzisha miradi
ambayo itawasaidia kupata fedha na mkaweza kujiendesha bila kutegemea
ruzuku kutoka serikalini, watumieni. Pale Dar es Salaam natazama yale
majengo ya magereza mnajengewa na jeshi wakati mngeweza kujenga
wenyewe.”
Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la
Kyela ASP. Nelson.M. Mwaifani amesema kwamba wao wamejitahidi
kuhakikisha kwamba gereza hilo halina msongamano wa mahabusu na kwamba
mazingira ya wafungwa na mahabusu ni mazuri salama kwa afya za watu hao
kwani wana mabweni na magodoro yanayowatosha wafungwa na mahabusu wote
waliopo katika gereza hilo. Pamoja na hayo ASP. Mwaifani amemwambia
Waziri Mahiga aliyeambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Biswalo
Mganga kwamba wameingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ya
kuzoa taka ngumu, kuzibua mifereji na kufanya usafi katika hospitali ya
Wilaya kwa makubalino ya kulipwa shilingi 6,700,000/- kwa mwezi.
Hata hivyo, Dkt. Mahiga
alifurahishwa na uongozi wa gereza la Kyela chini ya ASP. Nelson.M.
Mwaifani kwa kuwa wabunifu na kushirikiana vizuri na Halmashauri ya
Kyela kiasi cha kufanikiwa kupata tenda ya kufanya usafi katika
Halmashauri hiyo jambo linalowaingizia wastani wa cha shilingi milioni
sita kwa mwezi. Aidha aliwataka wakuu wote wa Magereza nchini kuiga
mfano huo na kwamba siku moja wawe sehemu ya taasisi za serikali
zitakazotoa gawio mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.
Dkt John Joseph Pombe Magufuli.
“Nataka siku moja gereza hili
lichangie kwenye mgao wa pesa za Taasisi ya Mahakama kwaajili ya gawio
la kwenda serikalini mbele ya Rais, nikisikia, nitafurahi sana. Nina
uhakika hivi karibuni tutaulizwa mchango wenu ni nini kwenye gawio la
serikali. Najua mnaweza kuwa vyanzo vingi vya kupata pesa hivyo ni
matumaini yangu kuwa gawio lijalo Wizara yetu au Taasisi ndani ya wizara
yetu itatoa kitu (‘very signficant’) kikubwa, na magereza nina uhakika.
Kule sabasaba kila mwaka mnapata zawadi tena nzuri tu, mnaongoza, sasa
hapa onesheni mfano mzuri.” Amesema Dkt. Mahiga.
Hivi Karibuni Mheshimiwa Rais Dkt.
John Joseph Pombe Magufuli azitaka Taasisi za Umma zinazozalisha na
kupata faida zitoe gawio kwa serikali na kuzipa siku 60
Taasisi,Mashirika na Makampuni ya serikali ambayo hajatoa yafanye hivyo
ndani ya muda huo. Waziri Mahiga ameamua kutumia ziara yake ya siku saba
pamoja na mambo mengine kuzipa changamoto Taasisi za utoaji haki jinai
kuanza kufikiria namna ya kuweka mikakati madhubuti ili nazo zianze
kutoa gawio kwa serikali. Ziara hii iliyoendelea leo katika Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Kyela na Gereza la Kyela, itaendelea tena kesho katika
Wilaya ya Mbarali jijini Mbeya.
No comments:
Post a Comment