Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula (katikati) akikagua risiti za malipo katika Kituo
cha Ukaguzi wa Madini cha Nala kilichopo Wilayani Dodoma Mjini katika
ziara yake yenye lengo la kukagua shughuli za madini ujenzi wilayani
humo tarehe 29 Oktoba, 2019.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Triple I
General Supply Limited, Maglan Kipuyo (katikati) akimwongoza Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto mbele) pamoja na
wataalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma na Tume
Makao Makuu kwenye machimbo yanayomilikiwa na kampuni yake yaliyopo
katika eneo la Mbalawala Wilayani Dodoma Mjini tarehe 29 Oktoba, 2019.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati) akitoa maelekezo
kwa Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano (kulia) kwenye ziara
yake katika machimbo ya mchanga yanayomilikiwa na Wema Msuya katika eneo
la Mundemu Wilayani Dodoma Mjini tarehe 29 Oktoba, 2019.
………………………..
Wachimbaji madini ujenzi waipongeza Tume ya Madini.
Na Greyson Mwase, Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula amefanya ziara Wilayani Dodoma Mjini lengo likiwa
ni kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya ujenzi pamoja na
kutatua
kero mbalimbali.
Katika ziara yake Profesa
Kikula aliambatana pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas
Mwano na maafisa kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini.
Mara baada ya kuwasili katika
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobass Katambi na kupokelewa
na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Michael Maganga, Profesa Kikula
alianza ziara yake kwa kutembelea kituo cha ukaguzi wa madini ujenzi
cha Nala kilichopo nje ya jiji la Dodoma na kutembelea baadhi ya
machimbo ya mchanga.
Akiwa katika machimbo ya
mchanga yanayomilikiwa na kampuni ya Tripple I General Supply Limited
yaliyopo katika eneo la Mbalawala, Wilayani Dodoma Mjini mara baada ya
kupokea taarifa ya uendeshaji wa shughuli zake, Profesa Kikula aliitaka
kampuni hiyo kuhakikisha inaandaa mkataba na kusaini kati yake na
wanakijiji wanaozunguka kampuni hiyo kwa ajili ya utoaji wa huduma za
jamii (corporate social responsibility) na kuepuka migongano.
“Ni vyema kampuni ikahakikisha
kunakuwepo na mkataba au muhtasari unaotambulika kisheria kwa ajili ya
makubaliano ya maeneo ambayo kampuni itasaidia kijiji katika kipindi
fulani kulingana na vipaumbele vya wananchi,” alisema Profesa Kikula.
Profesa Kikula alisisitiza kuwa,
ni vyema wananchi wakanufaika na rasilimali za madini kwa kupata huduma
za jamii kutoka kwa wawekezaji ikiwa ni pamoja na shule, vituo vya
afya, miundombinu, maji na kuendelea kusema kuwa kampuni inatakiwa
kuwashirikisha wananchi kwa kuwapa fursa ya kutoa huduma kwenye kampuni
kama vile vyakula, ajira.
Awali akitoa taarifa kwa
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi wa
Kampuni ya Tripple I General Supply Limited, Maglan Kipuyo alimpongeza
Mwenyekiti kwa ziara yake na kusisitiza kuwa kupitia ziara zake, kero
mbalimbali zimekuwa zikitatuliwa pamoja na kupewa elimu bora ya namna ya
kuchimba madini ya ujenzi kwa kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake.
Akielezea mafanikio ya kampuni
yake, Kipuyo alisema tangu kuanzishwa kwa kampuni mapema mwaka huu
kampuni imefanikiwa kutoa ajira zaidi ya 200, ununuzi wa mabati kwa
ajili ya ujenzi wa Ofisi ya kijiji cha Mbalawala na kuboresha
miundombinu ya barabara.
Alitaja mafanikio mengine kuwa
ni pamoja na malipo ya wastani wa shilingi milioni 15 kama mrabaha kwa
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma kwa kila mwezi na kuanza
kwa mchakato wa ujenzi wa kisima cha maji kitakachowanufaisha wanakijiji
wa Mbalawala.
Aidha, Kipuyo aliongeza kuwa
mafanikio mengine ni pamoja na kuwezesha wenye viwanda vidogo vya
kufyatulia matofali mkoani Dodoma kupata mchanga.
Katika hatua nyingine Profesa
Kikula alimtaka Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano kuendelea
kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini ya ujenzi kuhusu umuhimu wa kutoa
huduma kwa jamii (corporate social responsibility) kwa wananchi
wanaozunguka migodi yao kama Sheria ya Madini na kanuni zake
inavyofafanua.
Profesa Kikula pia alitembelea
machimbo ya mchanga yanayomilikiwa na Wema Msuya yaliyopo katika eneo
la Mundemu Wilayani Dodoma Mjini na kusisitiza umuhimu wa wachimbaji wa
madini ya mchanga kuchimba kwa kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake
pamoja kuzingatia suala la usalama na utunzaji wa mazingira.
“Mbali na kuchimba mchanga na
kulipa mapato Serikalini ni vyema mkahakikisha suala la usalama kwenye
shughuli zenu linazingatiwa na kuepusha ajali zinazoweza
kujitokeza,”alisema Profesa Kikula.
Naye Meneja wa machimbo hayo,
Richard Tairo mbali na kumpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa
Idris Kikula kwa kufanya ziara na kutatua changamoto mbalimbali mara
moja alimhakikishia ushirikiano kati ya wachimbaji wa madini ujenzi na
Serikali ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa
uchumi wa nchi.
Wakati huo huo Profesa Kikula
alitembelea viwanda vya kufyatulia matofali vilivyopo katika maeneo ya
Vyeyula na Mlimwa C Wilayani Dodoma Mjini ili kujionea namna shughuli
zinavyoendeshwa pamoja na ulipaji wa kodi Serikalini.
Profesa Kikula aliitaka Ofisi
ya Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma kusimamia kwa karibu zaidi na kuwa
wabunifu kwenye zoezi la ukusanyaji wa kodi mbalimbali ili Serikali
iweze kupata mapato yake stahiki.
No comments:
Post a Comment