Mkurugenzi mkuu wa
PSSSF, Hoseah Kashimba, (kushoto), akimhudumia mwanachama wa mfuko huo aliyekuwa
ametembelea banda katika Maonesho ya 43 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Sabasaba.
Na
Christian Gaya. Majira Ijumaa 02.Agosti.2019 www.majira.co.tz
WIKI iliyopita tuliona ya kuwa kwa
hapa Tanzania kulingana na sheria ya mfuko wa PSSSF namba 2 ya mwaka 2018
mfanyakazi ambaye ni mwanachama wa mfuko hukatwa asilimia 5 ya jumla ya mapato
yake yote kwa ...
mwezi na mwajiri analazimika huchangia asilimia 15 ya mshahara wa
mfanyakazi hivyo na kufanya kuwa jumla ya asilimia 20 na yote hupelekwa kwenye
akaunti ya mwanachama wa mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii. PSSSF ni mfuko
wa hifadhi ya jamii kwa ajili ya wafanyakazi wa umma.
Ambapo kuanzia Agosti Mosi, 2018, waliokuwa wanachama wa mifuko
iliyounganishwa yaani PPF, PSPF, LAPF, na GEPF waliohamishiwa katika mfuko wa
PSSSF wataendelea kuwa wanachama na kuchangia katika mfuko wa PSSSF.
Wakati kulingana na sheria ya
NSSF mfanyakazi ambaye ni mwanachama wa mfuko wa pensheni, hukatwa asilimia 10
ya jumla ya mapato yake yote kwa mwezi na mwajiri analazimika huchangia
asilimia 10 ya mapato yote ya mshahara wa mfanyakazi hivyo na kufanya kuwa
jumla ya asilimia 20 na yote hupelekwa kwenye akaunti ya mwanachama wa mfuko wa
pensheni wa hifadhi ya jamii.
Au mwajiri huweza kuchangia
asilimia 15 na mwajiriwa asilimia 5 au asilimia yote 20 inaweza kutolewa na
mwajiri kwa mfanyakazi wake kulingana na makubaliano kama sehemu ya motisha kwa
mfanyakazi wake. Ambapo mfuko huu wa NSSF ni kwa ajili ya wafanyakazi kutoka
katika sekta binafsi na sekta zisizorasmi. Na mwajiri haruhusiwi kumkata
mfanyakazi wake zaidi ya asilimia kumi ya mshahara wake.
Hivyo ni vema wanachama na wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii
kuwakumbusha kidogo juu sababu zilizofanya kuunganisha mifuko yote minne iliyoundwa
kisheria na kuzaliwa mfuko mmoja huu wa PSSSF.
Ikumbukwe ya kuwa mojawapo ya jukumu la mamlaka ya usimamizi
na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii (SSRA) ni kusimamia sekta ya hifadhi
ya jamii nchini. Ili kutimiza azma hiyo kifungu 135 cha Sheria Na. 5 ya mwaka
2012 kinaipa Mamlaka jukumu la kufanya tathimini ya hali ya sekta ya hifadhi ya
jamii kila baada ya miaka 3.
Hivyo SSRA iliingia mkataba na shirika la kazi duniani (ILO)
kwa lengo la kufanya tathimini ya mifuko ya hifadhi ya jamii. Tathmini hii
pamoja na mambo mengine ililenga kutekeleza mapendekezo ya wadau yaliyohitaji
kufahamu hali halisi ya Sekta, gharama za uendeshaji na kuunganisha mifuko ya
hifadhi ya jamii.
Kwa wakati huo kwa hapa Tanzania sekta ya hifadhi ya jamii ilikuwa
na mifuko saba ya msingi ambayo ni; mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF),
mfuko wa bima ya afya (NHIF), mfuko wa pensheni wa PSPF, mfuko wa pensheni wa
LAPF, mfuko wa pensheni wa PPF, mfuko wa mafao ya kustaafu wa GEPF pamoja na
mfuko wa fidia ya wafanyakazi (WCF).
Takwimu za sekta hii kwa kipindi
kinachoishia Juni 2015 zilionesha ya kuwa mifuko yote saba ilikuwa na jumla ya wanachama wapatao
milion 2.1 na jumla ya rasilimali zipatazo shilingi trilioni 8.78 wakati kwa
upande wa michango ni jumla ya shilingi trilioni 1.9. Na jumla ya mafao
yaliyolipwa kwa wanachama na wastaafu yalikuwa jumla ya shilingi trilioni 1.36
ambapo kwa upande wa uwekezaji ilikuwa jumla ya shilingi trilion 7.1.
Mpaka 2016 mifuko yote ilikuwa na jumla ya wastaafu wapatao 89,
532 nchini. Pia tathimini hiyo kutoka ILO ilionesha ya kuwa deni la pensheni
limepungua toka asilimia 58 ya pato la Taifa mwaka 2010 hadi asilimia 25 mwaka
2015.
Matokeo ya tathmini yalibainisha
kuwa umri wa kuishi baada ya kustaafu yaliongezeka kufikia miaka 20.8 kwa
wanaume, na miaka 22.2 kwa wanawake. Taarifa hiyo ilisema hali hii itaendelea
kuwa nzuri zaidi kadiri ya miaka inavyoongezeka ambapo kwa kipindi cha miaka 50
ijayo umri wa kuishi baada ya kustaafu kwa wanaume itakuwa miaka 22.9 na
wanawake miaka 24.9.
Thathmini hiyo ya ILO
ilionesha ya kuwa pensheni ilikuwa imeboreshwa kutoka wastani wa asilimia 67
hadi asilimia 72.5. Hata hivyo kwa mifuko inayolipa mkupuo wa asilimia 50
viwango vya pensheni kwa mwezi ilikuwa ni asilimia 27 ya mshahara. Taarifa
ilisema hiki kilikuwa kiwango cha chini sana, kwa sababu kiwango kinachotakiwa
kimataifa ni asilimia 40.
Pia ilionesha kwamba
kutumia mshahara wa mwisho kwenye kukokotoa mafao ni jambo linalokuwa linahitaji
kuangaliwa upya na kwa umakini mkubwa kwani una madhara makubwa kwa wanachama
wanaobaki kwenye mifuko.
Tathmini ilisisitiza
umuhimu wa kufanya uthaminishaji ili pensheni ziendane na ukuaji wa gharama za
maisha. Pia tathmini ilionesha kwamba kwa kiwango cha mkupuo wa asilimia 50
mifuko isingeweza kuthaminisha pensheni.
Na ilionesha kwamba mifuko imeimarika. Na kwamba mifuko ya
NSSF na PPF ilikuwa na uwezo kwa kustawi hadi kufika mwaka 2085 na 2075
Tathmini pia ilionesha kwamba mfuko wa LAPF na GEPF ilikuwa
na uwezo wa kufika zaidi ya mwaka 2058 na 2047. Na iwapo vikokotoo vyao
vingerekebishwa mifuko hii ingeweza kufika mwaka 2085.
Hali kadhalika iwapo mfuko wa PSPF ungepokea michango ya
kabla ya 1999 na kufanya marekebisho yanayopendekezwa kwa GEPF na LAPF mfuko
huu ungedumu hadi mwaka 2075.
Vilevile mfuko huu wa PSPF ulionesha kuimarika iwapo mafao yangerekebishwa
au michango kuongezwa hadi kufika asilimia 28 badala ya asilimia 20 kwa
kutegemea zaidi maamuzi ya wadau.
Kwa ujumla mifuko ilionekana kuwa na gharama kubwa ya
uendeshaji. Mfuko ambao ulikuwa wenye gharama ndogo ya uendeshaji ulikuwa PSPF.
Utafiti huo ulionesha ya kuwepo kwa gharama kubwa za
uendeshaji kama huu ungezorotesha utendaji wa mifuko. Ambapo nayo SSRA ilianza
kuandaa kanuni za kushusha gharama za uendeshaji.
Itaendelea
wiki ijayo
No comments:
Post a Comment