SPIKA
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametoa wito kwa
Serikali kuendeleza utalii wa Pwani ya Bahari ya Hindi, hatua
itakayosaidia kuchochea ukuaji wa utalii nchini.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa Jengo la tatu la abiria katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jana alhamisi (Agosti Mosi, 2019),
Ndugai alisema Tanzania ina kila sababu ya kuendeleza fukwe hizo
kutokana na ukweli kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi za fukwe na
bahari zilizo bora kuliko nchi yoyote ndani ya bara la Afrika.
Spika
Ndugai aliongeza kuwa uendelezaji wa fukwe hizo utasaidia nchi kwa
kiasi kikubwa kupiga hatua na kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025.
“Sisi
hapa Tanzania tuna pwani ya bahari nzuri zaidi kuliko pwani zingine
popote pale Afrika, hizi ni hifadhi za mwambao wa Pwani ya Bahari ya
Hindi, kuanzia Pangani mpaka Mtwara ambazo hazijatumika vizuri.” Alisema
Spika Ndugai
Aidha
Spika Ndugai aliongeza fukwe hizo zikitumika vizuri zitasaidia
kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kuoanishwa
vizuri kwa utalii wa pwani na ule wa bara na hivyo kuifanya sekta ya
utalii kuongeza wigo mwingine wa mtandao wa mapato nchini.
Akizitaja
sababu zilizopelekea utalii kutoonekana vizuri, Spika Ndugai alisema
moja ya sababu kubwa inayochangia sekta ya utalii kutokufanyika vizuri
ni kwa kuwa utalii wa fukwe za bahari bado uko chini ya Wizara ya
Mifugo na Uvuvi.
Aidha
katika kuonyesha umuhimu wa kuendeleza fukwe hizo, Ndugai aliyataja
maeneo ya Mombasa, Lamu na Malindi nchini Kenya kama maeneo ambayo
yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendeleza fukwe katika Pwani zao, ambapo
zimesaidia kuchochea ongezeko la watalii katika maeneo hayo.
“Kwenye
Pwani zao kwa sasa kuna utalii maarufu unaofanyika baharini,
unaofahamika kama ‘Marine Parks tourism’, ndio maana ukiangalia Pwani
yao imejaa hotel, na sisi hapa kwetu tukitumia fukwe zetu vizuri
tunaweza kuwa na utalii mzuri zaidi wa namna hii utakaosaidia kuongeza
idadi ya watalii nchini”. Alisema Spika Ndugai.
Pia
Spika Ndugai alimshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kuamua kuipandisha
hadhi iliyokuwa sehemu ya pori la akiba la Selous Game Reserve’ kuwa
hifadhi kamili itakayojulikana kama Hifadhi ya Taifa ya Nyerere au
‘Nyerere National Park’.
Akizungumzia
kuhusu suala hilo Rais Magufuli alisema pendekezo la kuendeleza fukwe
za pwani ya Bahari ya Hindi ni moja ya vipaumbele vya Serikali kwa
sasa, na kumuagiza Waziri Mkuu , Kasim Majaliwa kuangalia jinsi ya
kuendeleza fukwe zote kuanzia Moa hadi Msimbati.
MWISHO
No comments:
Post a Comment