Pages

Friday, August 30, 2019

POLISI TANZANIA YANYAKUA MEDALI 29 KATIKA MICHEZO YA EAPCCO 2019 KENYA


Wachezaji wa timu ya Polisi Tanzania wakiwa katika picha ya Pamoja kabla ya mechi kuanza katika viwanja vya Kasarani jijini Nairobi nchini Kenya.
Wahamasishaji kutoka Jeshi la Polisi wakishangilia timu ya Jeshi la Polisi ikiwa inacheza mpira wa miguu na timu ya Polisi Burundi ambapo Tanzania iliibuka mshindi kwa kuifunga Burundi bagoli 2 kwa 1.
Mwanariadha wa  Polisi Tanzania katika mbio za nyika WP. Catherine akiwa katika mbio hizo katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Kenyata jijini Nairobi,  nchini Kenya ambaye ameiwezesha nchi ya Tanzania kuingia katika  nafasi ya pili katika mashindano ya michezo ya  EAPCCO 2019.
Mwanariadha wa  Polisi Tanzania PC Michael  baada ya kumaliza mbio za mita 100 katika viwanja vya Kasarani jijini Nairobi,  nchini Kenya na kuiwezesha nchi ya Tanzania kuingia katika  nafasi ya pili katika mashindano ya michezo ya  EAPCCO 2019.
…………………
Timu za Jeshi la Polisi Tanzania zinazoshiriki katika michezo ya Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kanda ya Afrika Mashariki (EAPCCO 2019) inayochezwa katika viwanja vya
Kasarani na Chuo Kikuu cha Kenyata, jijini Nairobi nchini Kenya zimefanikiwa kupata jumla ya Medali 29. Katika medali hizo dhahabu 2, Silva 7 pamoja na Medali 20 za Shaba.
Medali hizo zimepatikana katika michezo mbalimbali ikiwemo, Judo, Taekwondo, Kareti, mchezo wa kurusha vishale, Riadha, mchezo wa Kurusha kisahani, kuruka vihunzi, mpira wa miguu, mpira wa kikabu, kulenga shabaha, kuvuta kamba pamoja na mpira wa wavu.
Katika mchezo wa Taekwondo mchezaji wa Tanzania Omary Ramadhani ambaye pia  ni Mkufunzi katika Shule ya Polisi Moshi (TPS) aliibuka mshindi kwa kumpiga Mkenya na kufanikiwa kuingia fainali.
Aidha, katika michezo ya mbio za nyika, Timu ya Kenya imeshika nafasi ya kwanza, Tanzania imeshika nafasi ya mbili, Uganda nafasi ya tatu ambapo Sudani ya kusini ikishika mkia kwa kupata nafasi ya nne.
Michezo hiyo ya Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za kanda ya Afrika Mashariki (EAPCCO 2019) inajumuisha nchi 14 ambapo kati ya hizo nchi 7 zipo katika mashindano hayo. Nchi hizo ni Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani, Sudani ya Kusini pamoja na nchi ya Kenya ambayo ndio mwenyeji wa michezo hiyo.
Michezo hiyo ya EAPCCO 2019  ilifunguliwa na  Waziri  wa Usalama wa Ndani, Dkt. Fred Matiangi katika viwanja vya Kasarani jijini Nairobi nchini Kenya ambapo aliwataka nchi  washiriki wa michezo  ya EAPCCO kuimarisha ushirikiano, uhusiano pamoja na kupanua wigo wa mawasiliano miongoni mwa nchi wanachama ikiwa ndio lengo kubwa la muungano huo.
Dkt. Mataiangi amewahimiza nchi wanachama wa EAPCCO kujikita katika kutekeleza mikakati ya kupambana na uhalifu kwa kubadilisha uzoefu na taaarifa za kiitelijensi kikanda.
Pia, alisisitiza kuwa mikakati hiyo itoe kipao mbele katika kubaini, kuzuia, kupambana na kupeleleza makosa yanayovuka mipaka kama vile uhalifu wa kimtandao, usafirishaji haramu wa binadamu, wizi wa magari pamoja na uhalifu wa mazingira.
Michezo hiyo ya  Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kanda ya Afrika Mashariki (EAPCCO 2019) imeingia siku ya nne tangu kufunguliwa ambapo inatarajiwa kufikiwa kilele chake septemba 2, 2019.

No comments:

Post a Comment