Na Mwandishi Wetu, MOHA
NAIBU
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima,
amelitaka Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kuboresha mazingira ya huduma
wanazotoa kwa wananchi.
Alisema
ni wajibu wa jeshi hilo kutoa elimu kwa jamii iweze kufahamu hatua za
kufuata pindi wanapotaka kuwawekea dhamana ndugu zao waliopo katika
vituo vya polisi.
Kailima aliyasema hayo hayo jana alipofanya ziara ya kutembelea vituo vinne vya polisi mkoani Dodoma.
Lengo
la ziara hiyo iliyoandaliwa na Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko
Ndani ya Wizara hiyo ni kuangalia utendaji kazi wa jeshi hilo juu ya
huduma wanazotoa kwa wananchi.
Vituo
alivyotembelea ni vile vilivyopo katika Wilaya ya Dodoma Mjini ambavyo
ni Kituo Kikuu (Central), Chang’ombe, Nkuhungu na Kikosi cha Usalama
Barabarani.
Katika
ziara hiyo, Kailima aliambatana na Mkurugenzi wa Kitengo cha
Kushughulikia Malalamiko, Kamishna wa Polisi, Albert Nyamuhanga pamoja
na Maafisa wengine wa kitengo hicho.
Akiwa
kwenye kituo Kikuu cha Polisi (Central), Kailima alikuta idadi kubwa ya
watu waliokuwa na shida mbalimbali, alitumia fursa hiyo kuzungumza nao
na kuwataka waeleze kero zao.
Baada
ya kuzungumza na wananchi, Kailima aliushauri uongozi wa kituo hicho
kuweka mazingira mazuri ya kutoa huduma ili kuondoa mrundikano wa
wananchi nje, ndani ya kituo.
“Wekeni
mazingira mazuri ya mwananchi mmoja kuhudumiwa na askari mmoja kutokana
na idadi ya askari ambao watakuwa zamu ili kupunguza msongamano,”
alishauri.
Aliongeza
kuwa; “Toeni elimu inayohusu dhamana kwa jamii ili wananchi wajipange
kabla ya kuja kituoni, unakuta watu wengi wanakuja kuwawekea dhamana
ndugu zao bila kujua taratibu hivyo kusababisha wajazane kituoni bila
sababu,” alisisitiza.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Dodoma, Pipi Kayumba, alisema
katika utendaji kazi wake, kila siku anapita kituoni hapo ili kuonana na
wananchi anaowakuta kituoni, kusikiliza shida zao.
Alishauri
ili jeshi hilo liweze kuboresha huduma zake, kuwepo vituo vya polisi
katika njia zote za kuingia jijini Dodoma kwani jiji hilo limekuwa
kubwa, idadi ya watu imeongezeka.
“Kwa
sababu ya ongezeko kubwa la watu, hata utoaji huduma nao umekuwa
mkubwa, kuanzishwa kwa vituo hivyo litakuwa jambo jema kwa Jeshi la
Polisi na nchi kwa ujumla,” alisema.
Kwa
upande wake, Kamishna Nyamuhanga alishauri Mkuu wa Kituo hicho, Kidwadi
Karinga, aweke mkakati wa kuondoa malalamiko ya wananchi kwenye kituo
hicho.
Kailima
aliendelea na ziara yake kwenye Kituo cha Kikosi cha Usalama
Barabarani, kuzungumza na wananchi waliodai kuna mtu ambaye si askari
alikuwa akitoa taarifa ya upotevu wa mali (loss report).
Mtu
huyo alikuwa akitoa taarifa hiyo nje ya kituo hicho kwa gharama kubwa
wakati gharama halisi ni sh. 500 tu, hulipwa kwa utaratibu uliowekwa na
kupewa lisiti.
Kailima
alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa lengo la ziara hiyo ni
kujionea mazingira ya kazi za askari kwa jamii ili kupunguza malalamiko
kutoka kwa wananchi.
Alimpongeza
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Nuru Selemani kwa
kutekeleza agizo la Waziri wa Wizara hiyo, Kangi Lugola juu ya
kuziondoa pikipiki zilizokamatwa kwa makosa mbalimbali.
“Wasisitize
askari wako waache kuomba na kupokea rushwa, kutobambika kesi kwa
wananchi, askari kutumia lugha nzuri, kuelimisha wananchi wanapofanya
kosa, kutoa elimu katika redio namna ya kuvuka kwenye zebra, kutoa
taarifa kuhusu hali ya mji kila siku,” alisisitiza Kailima.
Aliwataka
askari wa Usalama Barabarani wafanye operation kubwa mara moja kwa
mwezi ili kufanya wepesi wa kukusanya maduhuli ya serikali, kutimiza
wajibu wao wawapo kazini na wanaokwenda tofauti wachukuliwe hatua
stahiki.
Alisisitiza
suala la usalama hasa kipindi hiki ambacho kuna ugeni wa Mkutano wa
SADC kuanzia Agosti 5, mwaka huu, hivyo kama chombo cha usalama wamuunge
mkono Rais Dkt. John Magufuli.
Pia
Kailima alitembelea Kituo cha Chang’ombe kinachohudumia kata tatu za
Chamwino, Chang’ombe na Chinangali ambapo hali ya usalama si nzuri
kutokana na matukio ya wizi, unyang’anyi.
Matukio hayo yamelifanya jeshi hilo kufanya msako mkali na tayari baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.
Kailima aliushaurio uongozi wa kituo hicho na askari kuitumia jamii au serikali za mitaa ili kupata taarifa za wahalifu.
Mkuu
wa kituo hicho, Emanuel Mawi, alisema kuna doria inafanyika maeneo
mbalimbali, pia wanashirikiana na jamii, changamoto waliyonayo ni udogo
wa kituo ambacho kinahudumia eneo kubwa.
Akiwa kwenye Kituo cha Nkuhunga, Kailima aliambiwa kituo hicho kinahudumia kata mbili za Nkuhungu na Kizota.
Akiwa kituoni hapo, Kialima aliambiwa kituo hakilazi mahabusu ambao hupelekwa Kituo Kikuu (Central).
Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Dodoma, Kayumba alisema changamoto waliyonayo ni uchache wa magari kwa ajili ya doria za kila siku.
Kailima aliwapongeza Kayumba na Karinga kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Kwa
upande wake, Kamishna Nyamuhanga, alimshukuru Kailima na kumuahidi
kuwa, watatekeleza maelekezo yote aliyotoa katika ziara hiyo ili
kuboresha utendaji kazi.
No comments:
Post a Comment