Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga
(Mb) amesema kuwa Kutokana na ushindani wa zabuni za BPS iliyofunguliwa Juni
21, 2019, bei za mbolea ya DAP katika chanzo ilipungua kwa asilimia 12
ikililinganishwa na bei za zabuni ya Julai, 2018. Sambamba na punguzo
lililotokana na zabuni hiyo, Serikali ilifanya marejeo ya kikokotoo cha bei
elekezi ambacho kimetumika kwa misimu ya kilimo 2017/2018 na 2018/2019.
Waziri Hasunga ameyasema hayo leo
tarehe 28 Agosti 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisi ndogo za
wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa Ushindani wa zabuni za
BPS pamoja na marejeo ya kikokotoo umefanya bei ya mbolea kwa mkulima kupungua kwa wastani kimkoa wa Tshs 8,000/=
hadi Tshs 10,000/ sawa na asilimia 13 - 17 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea aina
ya DAP.
Aidha, punguzo la Tshs 5,000/= 6,000/= sawa na asilimia 14 – 19 kwa
wastani wa kimkoa kwa mfuko wa kilo 25. Kwa mfuko wa kilo 5, bei imepungua kwa Tshs 1,300/= 1,500/= sawa na asilimia
15 – 20 wastani wa kimkoa.
Kwa muktadha huo, bei elekezi ya
mbolea ya DAP kwa mikoa ya Kanda ya Mashariki, Kati, Kusini na Kaskazini
zitakuwa kati ya Sh. 51,900/= na
60,300/=. Aidha, kwa mikoa ya Kanda ya Magharibi, Nyanda za Juu Kusini na
Ziwa, bei elekezi itakuwa kati ya Sh.
57,000/= na 63,200/=. Bei hizi zitaanza kutumika rasmi tarehe 1 Septemba, 2019 na zitaendelea
kutumika hadi pale itakapotangazwa bei nyingine.
Mhe Hasunga amesema kuwa bei hizo ni
kikomo cha juu kwa Mkulima katika eneo husika. Hivyo, wafanyabiashara wanaweza
kuuza chini ya bei elekezi bila kuathiri
ubora wa mbolea. Kwa kuzingatia hilo, Wizara imetoa bei elekezi ya jumla na
rejareja za mbolea kwa uzani wa kilo 50, 25, 10 na 5.
Alisema kuwa ni kosa kisheria kuuza
mbolea kwa bei ya juu ya bei kikomo kwa nia ya kujiongezea kipato.
Alisema ili kumwezesha mkulima mdogo
kupata mbolea hizi zikiwa katika hali ya ubora unaokubalika, Wizara imetoa pia
bei elekezi ya jumla na rejareja za mbolea kwa uzani wa kilo 50, 25, 10 na 5.
Hivyo, wakulima wanashauriwa kununua mbolea katika mifuko maalum.
Endapo kutakuwa na tofauti ya gharama
za usafirishaji kwa baadhi ya sehemu katika baadhi ya maeneo ambayo itakuwa
haiendani na bei elekezi, maelekezo ya suala hili yatatolewa kwa Wakuu wa
Mikoa/Wilaya kuwapa Mamlaka ya kukaa na Kamati za pembejeo na kurekebisha bei
elekezi ili ziendane na hali halisi kwa kuzingatia jiografia ya eneo husika ili
kurahisisha usambazaji na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima.
Mhe Hasunga alisema kuwa bei elekezi za mbolea hutegemea
umbali wa sehemu inakopelekwa kutokea bandarini. Maeneo yote itakapopelekwa
mbolea yana umbali kati ya kilometa 1 na 1,600 kutoka bandari ya Dar es salaam.
Kwa Wastani, gharama ya kusafirisha mfuko mmoja wa mbolea
wa Kilo 50 kwa barabara kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi makao makuu ya
Halmashauri kwa barabara ni Sh. 5,500/= kwa kilometa 1,000. Gharama hii hupanda
na kushuka kutegemeana na hali ya barabara na hali ya hewa (masika au
kiangazi).
Aidha, usafiri kwa njia ya Reli ni nafuu zaidi kwa sababu
gharama za kusafirisha mbolea kwa kilometa 1,000 kwa mfuko wa kilo 50 ni Tshs 4,160 (TRC) au Tshs 4,600 (TAZARA).
Katika kuhakikisha kwamba tija ya
uzalishaji wa mazao ya kilimo inaongezeka kwa ajili ya kujitosheleza kwa
chakula na kutoa malighafi za viwandani; Wizara ya Kilimo imeendelea
kuhamasisha matumizi ya mbolea ili kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta
moja kama ilivyopendekezwa na wakuu wa nchi za Afrika kupitia Azimio la Abuja
la mwaka 2006.
Waziri huyo wa Kilimo Mhe Japhet
Hasunga amesema kuwa ili kufikia lengo hilo serikali ilianzisha Mfumo wa
Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS - Bulk
Procurement System), kufuta tozo mbalimbali za mbolea, kusimamia utaratibu
wa usafirishaji wa mbolea na kuweka bei elekezi za mbolea kwa mkulima.
Uingizaji wa mbolea kupitia BPS
unahusu mbolea za Urea, DAP, NPK, CAN na SA. Hata hivyo, kwa sasa BPS inatumika
kuingiza mbolea za DAP na Urea ambazo zinazotumika kwa zaidi ya asilimia 50.
No comments:
Post a Comment