
Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umewataka watu ambao sauti zao
zimedukuliwa na kusambazwa mitandaoni kufungua kesi mahakamani.
Mratibu
wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo
Olengurumwa, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu ushauri wa hali ya faragha na usalama wa
mawasiliano.
"Suala
la mawasiliano binafsi limelindwa kikatiba na kisheria kama haki ya
faragha, zipo mamlaka ambazo zimeruhusiwa na sheria kuweza kuchukua
taarifa binafsi za mtu kwa matumizi maalamu lakini hazipaswi kubadilika
kuwa za umma," alisema Olengurumwa.
Kauli
hiyo ya THRDC imekuja zikiwa siku chache baada ya Mbunge wa Ubungo
(Chadema), Saeed Kubenea, kutaka TCRA kuwachukulia hatua wanaohusika na
vitendo hivyo vya udukuzi.
Kubenea
alisema hayo baada ya kudaiwa kuwa mawasiliano Mbunge wa Mtama, Nape
Nnauye na makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuph
Makamba, yamedukuliwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Jambo
hilo lilibuka baada ya Kinana na Makamba kumwandikia barua Katibu wa
Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, Pius Msekwa,
wakilalamikia kile walichodai kuwa wamedhalilishwa na mwanaharakati
Cyprian Musiba.
Olengurumwa
alisema serikali inapaswa kutunga sheria hiyo ili kuepusha ukiukwaji wa
haki ya faragha itakayoendana na Katiba ya Tanzania na mikataba mingine
ya kimataifa kuhusu haki ya faragha na mawasiliano.
Alisema
kifungu cha 16 (1) cha Katiba ya Tanzania kinaeleza kuwa: "Kila mtu
anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake
binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya
maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi."
Pia
alisema THRDC inawataka watoa huduma za mawasiliano kuhakikisha
wanalinda heshima ya biashara zao kwa kulinda taarifa za faragha za
wateja wao na kwamba wananchi ambao haki zao za faragha zimevunjwa
wanapaswa kwenda kufungua kesi mahakamani.
"Watu
wote ambao haki yao ya faragha imevunjwa, wanahimizwa kufungua kesi
katika Mahakama Kuu Kanda yoyote nchini, kuwashtaki watoa huduma au watu
binafsi walioingilia kwa namna yoyote kudukua na kutumia mawasiliano
hayo bila hati ya ruhusa ya mahakama," alisema Olengurumwa.
Alisema
watu hao wanaweza kwenda kufungua kesi na kushtaki watoa huduma za
mawasiliano kwa kuwa ni kosa kuvujisha mawasiliano ya mtu bila ya
lidhaa.
No comments:
Post a Comment