Waziri
wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na waandishi wa habari
kutoka vyombo mbalimbali mkoani Morogoro, kuhusu maandalizi ya uwekaji
jiwe la msingi la ujenzi mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko
ya maji ya Mto Rufiji, unaotarajiwa kufanyika Julai 26, 2019.
Baadhi
ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (hayupo pichani) na waandishi wa habari wa Morogoro (hawapo
pichani) kuhusu maandalizi ya hafla ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa
mradi wa umeme wa Rufiji, unaotarajiwa kufanyika Julai 26, 2019.
Matukio
mbalimbali wakati Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alipokuwa
akikagua maandalizi hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi mradi wa
kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji,
unaotarajiwa kufanyika Julai 26, 2019.
Na Veronica Simba – Pwani
Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, amewasihi watanzania kuwa wazalendo
kwa kuacha kuuita mradi wa kuzalisha umeme kwa maporomoko ya maji ya mto
Rufiji kwa jina la Stiegler’s badala yake wauite kwa jina lake halisi
la kizalendo.
Aliyasema
hayo kwa nyakati tofauti jana, Julai 24, 2019 wakati akizungumza na
waandishi wa habari mkoani Morogoro na baadaye akiwa Rufiji mkoani Pwani
mara baada ya kutembelea na kukagua maandalizi ya uwekaji jiwe la
msingi la ujenzi wa mradi huo, unaotarajiwa kufanywa na Rais John Pombe
Magufuli, kesho, Julai 26.
“Jina halisi ni Mradi wa Umeme wa Rufiji na siyo Stiegler’s kama ambavyo wengi wamekuwa wakiuita. Nawasihi watanzania kuenzi jina la utaifa la Rufiji,” alisisitiza Waziri.
Akizungumza
katika maeneo hayo tajwa, Dkt. Kalemani alisema utekelezaji wa mradi
husika, utaweka mazingira sahihi, yanayotabirika na imara katika kujenga
uchumi wa viwanda.
Akifafanua,
alisema hiyo ni kutokana na Sera na Dira ya Taifa ya kujenga uchumi wa
viwanda, lakini pia kuinua maisha ya watanzania kutoka kima cha chini
kwenda kima cha kati ifikapo mwaka 2025.
Alisema,
lengo kubwa la mradi husika; pamoja na mambo mengine, ni kuzalisha
umeme wa kutosha, wa uhakika, unaotabirika na wenye gharama nafuu.
“Tumpongeze
sana Mheshimiwa Rais wetu kwa umahiri mkubwa wa utekelezaji wa mradi
huu. Kwa niaba ya Wizara ya Nishati, nataka kuwahakikishia watanzania
kuwa mradi huu utatekelezeka kwa wakati na upo uwezekano wa kuokoa walau
mwezi mmoja wa ukamilishaji wake kimkataba.”
Akizungumzia
manufaa makubwa mengine ya mradi, alisema ni pamoja na ajira ambapo
alieleza kuwa hadi sasa watanzania 600 wameajiriwa kwa shughuli za awali
za ujenzi. Aliongeza kuwa, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kufikia
6,000 na zaidi pindi mradi utakapofikia katika kilele cha ujenzi wake.
Waziri
alieleza manufaa mengine kuwa ni uunganishaji wau meme katika maeneo
yaliyo jirani na mradi ambapo alisema jumla ya vijiji 22 vya mikoa ya
Morogoro na Pwani tayari vimeshanufaika na kwamba vijiji vingine 37 vya
mikoa hiyo vitapatiwa umeme baada ya kujenga miundombinu ya
kuusafirisha.
Vilevile
alitaja manufaa mengine kuwa ni pamoja na kuwezesha kilimo cha
umwagiliaji, uvuvi pamoja na kuwezesha uhifadhi wa mazingira kutokana na
kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mkaa yanayosababisha ukatwaji
wa miti.
Aliwaasa
wananchi kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea eneo la mradi ili
kujionea na kujifunza, kabla watalii kutoka nchi mbalimbali duniani
hawajaanza kuja kutalii eneo hilo.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephen Kebwe alimpongeza
Waziri wa Nishati kwa jitihada ambazo Wizara imeendelea kufanya katika
utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji.
Alisema
mradi utaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kama
yalivyoelezwa na Waziri lakini pia akamhakikishia Dkt. Kalemani kuwa
suala la ulinzi na usalama katika eneo la mradi limezingatiwa kwa uzito
wa aina yake.
“Tumeongeza
idadi ya askari Polisi ili kudhibiti kikamilifu tukio lolote la
kihalifu endapo litajitokeza. Hata hivyo, hadi sasa hatujapata shida
yoyote ya kiusalama,” alisema.
Mkutano
wa Waziri na waandishi wa habari ulihudhuriwa pia na Kaimu Kamishna wa
Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa Idara
ya Habari – MAELEZO, Dkt Hassan Abbas pamoja na wataalamu mbalimbali wa
Wizara na TANESCO.
No comments:
Post a Comment