Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akisalimiana na Rais wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina alipomtembelea ofisini kwake
kwa ajili ya mazungumzo maalum, baada ya Mkutano wa Mawaziri wa Fedha
wa nchi za Afrika Mashariki, Abidjan, Ivory Coast
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki
ya Maendeleo ya Afrika Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Gabriel Negatu,
muda mchache kabla ya kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, Abidjan, Ivory Coast.
Washiriki wa Mkutano wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Rais
Mwandamizi wa AfDB, Bw. Charles Boamah, Abidjan nchini Ivory Coast.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akichangia mada katika Mkutano wa Mawaziri
wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki na Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, uliofanyika Abidjan, Ivory Coast,
kulia ni Katibu Mkuu wa Benki hiyo, Prof. Vicent Nmehielle.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akijadili jambo na Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, baada ya Mkutano wa
Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki na Rais huyo, Abidjan,
Ivory Coast.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya
pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Dkt. Akinumwi
Adesina na baadhi ya wajumbe wa benki hiyo, baada ya kikao maalum cha
Mhe. Mpango na Rais huyo, Abidjan, Ivory Coast.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (ADB), Dkt. Akinumwi Adesina, na baadhi ya Mawaziri
wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki waliohudhuria Mkutano wa Kikanda wa
Mawaziri wa Fedha na Rais huyo, Abidjan, Ivory Coast.
(Picha na Farida Ramadhani-WFM, Abidjan, Ivory Coast)
…………………………….
Na Farida Ramadhani, WFM, Abidjan
Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika
kutekeleza
miradi mbalimbali ya maedeleo ikiwemo mindombinu ya barabara, umeme na
ujenzi wa viwanja vya ndege hususan Kiwanja cha Msalato mkoani Dodoma.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, baada ya kukutana na kufanya
mazungumzo na Rais wa AfDB, Dkt. Akinwumi Adesina, wakati wa Mkutano
wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki, uliofanyika Abidjan
nchini Ivory Coast.
Dkt. Mpango, ambaye pia ni Gavana
wa Benki ya Maendelo ya Afrika (AfDB), alisema Rais wa Benki hiyo
amekubali ombi la Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli la kuipatia
Tanzania mkopo nafuu ili kuwezesha kuanza ujenzi wa kiwanja cha ndege
cha Msalato mkoani Dodoma.
“Benki hii imekuwa ni ya msaada
mkubwa sana na yapo maeneo mengi ambayo Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika amekubali kuendelea kushirikiana na nchi yetu”, alisema Mhe.
Mpango.
Mhe. Mpango alieleza kuwa Dkt.
Adesina ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais
Dkt. Magufuli, kwa juhudi zake za kupiga vita rushwa, ufisadi na
ubadhirifu wa mali za umma kwa vitendo, kufanya maamuzi magumu ya
kulinda rasilimali za Taifa hususan madini, kudhibiti matumizi yasiyo ya
lazima Serikalini, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti
ukwepaji kodi.
Alisema kuwa Dkt. Adesina ameahidi
kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
ambazo zimesababisha Tanzania kupata mafanikio makubwa katika maendeleo
kwa kipindi kifupi.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa
Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki, Mhe. Mpango aliishukuru
Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kuendelea kuipatia mikopo nafuu kwa
ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
Katika mkutano huo wa Mawaziri,
Mhe. Mpango aliuomba uongozi wa Benki kuharakisha maandalizi ya miradi
inayotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2019 ikiwemo: Ujenzi wa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa Msalato (USD milini 200); Ujenzi wa Barabara ya
Kuzunguka Jiji la Dodoma (USD milioni 180).
Miradi mingine ni Mradi wa Kufua
Umeme wa Maji (87 MW) wa Kakono (USD milioni 350); Ujenzi wa Barabara ya
Bagamoyo-Tanga/Lungalunga-Mombasa-Malindi (USD milioni 158.2); na Awamu
ya Pili ya Mpango wa Kuendeleza Utawala Bora na Maendeleo ya Sekta
Binafsi (USD milioni 56).
Benki ya Maendeleo ya Afrika
imeahidi kuiwezesha Tanzania kupata mikopo nafuu ili miradi hiyo iweze
kuanza kutekelezwa mapema. Aidha, iliahidi kuwa mkataba wa Dola za
Marekani milioni 256 kwa ajili ya ujenzi ya barabara ya
Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) kwa kiwango cha lami utasainiwa mapema
mwanzoni mwa mwezi machi, 2019.
Kwa upande mwingine, Mawaziri wa
Fedha wa nchi za Afrika Mashariki waliohudhuria mkutano huo,
walimuahidi Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kuwa wataendelea kuunga
mkono kusudio la Benki hiyo la kuongeza mtaji ili kuziwezesha nchi
wanachama kupata mikopo nafuu kwa ajili kutekeleza miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment