Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi akihutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za
Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
maofisa wa Tanzania mara baada ya kuhutubia kikao hicho cha Baraza la
Haki za Binadamu jijini Geneva Uswissi.
……………………………………………………………………………….
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu na ustawi
wa
jamii kama kipaumbele chake na itaendelea kushirikiana na Baraza
hilo kuhakikisha haki za binadamu nchini na duniani kote zinadumishwa.
Prof. Kabudi amesema hayo
alipolihutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa
Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.
Prof. Kabudi amesema Serikali ya
Tanzania imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha haki za binadamu,
utawala bora na utii wa sheria nchini na kuondoa ukatili dhidi ya
wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
“Serikali imelenga kuimarisha
haki za binadamu, utawala bora, utii wa sheria na kuondoa ukatili dhidi
ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, kwa sasa tunatekeleza mpango
mkakati wa kitaifa wa kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa
mwaka 2017/18 – 2021/22, lengo likiwa ni kulinda na kudumisha haki za
wanawake, watoto na watu wenye ulemavu,” alisema Prof. Kabudi.
Amesema Serikali pia inazingatia
suala la kuwapatia haki kwa haraka wananchi wasio na uwezo kwa kutolea
maamuzi kwa haraka mashauri yanayowahusu watu wasio na uwezo na
kuwapatia msaada wa kisheria kupitia utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa
Kisheria ya mwaka 2017 ili wananchi hao waweze kupata haki zao kwa
wakati.
Aidha, Prof. Kabudi
amelihakikishia Baraza hilo kuwa Serikali inatambua kazi kubwa
inayofanywa na vyombo vya habari nchini na imeendelea kuhakikisha uhuru
wa vyombo hivyo unalindwa huku jumla ya vituo vya redio 152, televisheni
34, magazeti 172 nchini kote yamesajiliwa na kuongeza kuwa Serikali
itaendelea kuweka mazingira stahiki yatakayowezesha vyombo vya habari
kufanya kazi zao kwa uhuru.
Ameongeza kuwa Serikali
imedhamiria kuleta ustawi wa jamii kwa kutekeleza mipango mbalimbali ya
maendeleo ikiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 na
kunadi kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya
kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote.
“Tanzania imepiga hatua kubwa
katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji zinawafikia
wananchi wote na kuongeza kuwa Serikali inatumia zaidi ya Shilingi
Bilioni 23 kwa mwezi kutoa elimu pasipo malipo na hivyo kuongeza udahili
wa watoto wanaojiunga darasa la kwanza kwa asilimia 35.2 na asilimia
20.1 kwa wanaojiunga na kidato cha kwanza,” alisema.
Prof. Kabudi pia amesema Serikali
imedhamiria kufikisha huduma za afya karibu na watanzania wote ambapo
imeongeza bajeti ya afya kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi
Shilingi bilioni 269 mwaka 2017/2018 na kuongeza kuwa Serikali
inatekeleza mikakati ya kujenga vituo vya afya ambapo hadi sasa imejenga
vituo 304, na nyumba za watumishi wa afya 578 zimejengwa nchini kote.
Baraza la Haki za Binadamu la
Umoja wa Mataifa ni chombo cha Umoja wa Mataifa chenye jukumu la kukuza
na kulinda haki za binadamu duniani kote na kushughulikia uvunjwaji wa
haki za binadamu unaotokea katika nchi wanachama wa umoja huo na
kushauri hatua za kuchukuliwa ili kuboresha haki za binadamu duniani.
Baraza hilo pamoja na mambo
mengine linatarajia kupokea taarifa mbalimbali kuhusu haki za binadamu
duniani na kutoa nafasi kwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa kutoa maelezo yao kuhusu utekeelezaji wa wajibu wao wa kulinda
na kukuza haki za biandamu katika nchi zao.
No comments:
Post a Comment