Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
Zanzibar Bi. Asha Ali Abdulla akikabidhiana mkataba wa Matibabu kwa
wagonjwa kutoka Zanzibar na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya
Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Respicious Bonifece katika Hafla
iliyofanyika Zanzibar Januari 31, 2019.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
Zanzibar Bi Asha Ali Abdulla akitia saini mkataba wa wagonjwa kutoka
Zanzibar kupata huduma za kibingwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili
(MOI)
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Respicious Boniface akitia saini
mkataba wa wagonjwa kutoka Zanzibar kupata huduma za kibingwa za Taasisi
hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
Zanzibar Bi. Asha Ali Abdulla akizungumza na waandishi wa habari
(Hawapo pichani ) katika hafla ya utiaji saini Januari 31, 2019
Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Respicious Boniface akizungumza na
waandishi wa habari (Hawapo pichani ) katika hafla ya utiaji saini
iliyofanyika Zanzibar leo.
Mwanasheria wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Bw. Suleimani Mgerwa akitia saini Mkataba huo leo mjini Zanzibar.
- Mwanasheria wa Wizara ya Afya Zanziba Bi. Shufaa Nassoro Ali akitia sini Mkataba huo leo mjini Zanzibar.
(Picha zote na MOI)
…………………….
Na; Mwandishi wetu- MOI
Wizara ya Afya ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar imesaini mkataba na Taasisi ya Tiba ya Mifupa
Muhimbili (MOI) utakaowezesha wagonjwa kutoka Visiwani humo kupata
matibabu ya kibingwa waliyokuwa wakiyapata nje ya nchi kwa gharama
kubwa.
Utiaji saini wa mkataba huo
umefanywa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi Asha Ali. Abdulla pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface leo mjini Zanzibar.
“Tumekuwa tukipeleka wagonjwa
wengi nje ya nchi kwa matibabu hususan hawa wa mifupa, sasa tunafahamu
kwamba wenzetu wa MOI wameboresha sana huduma zao hivyo tumeamua
wagonjwa wetu waende MOI badala ya kwenda nje, naamnini Mashirikiano
hayo haya yatakuwa yenye tija kwa wananchi wetu” alisema Bi Asha.
Asha ameongeza kwamba wagonjwa
wamekuwa wakienda MOI kupata huduma kwa kipindi kirefu lakini mkataba
huu unafanya ushirikiano uwe rasmi na wagonjwa wapokelewe na kupata
huduma kwa namna bora zaidi.
“Hili siyo jambo jipya, wagonjwa
wetu wanakuja huko kupata huduma na tunashukuru kwamba mmekuwa
mkiwahudumia vyema, mkataba huu utaboresha namna mnavyowapokea na hata
kama kutakuwa na changamoto yoyote kwa mgonjwa tutajadiliana na
kuangalia nini cha kufanya kwani mambo sasa yamekuwa rasmi” Alisema Bi
Asha
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema ni heshma kubwa kwa MOI
kuingia mkataba na Wizara ya Afya ya Zanzibar ikiwa ni ishara tosha
kwamba Serikali ya Zanzibar imetambua maboresho yaliyofanyika MOI pamoja
na huduma za ubora wa hali ya juu zinazotolewa.
” Tunawashukuru sana kwa kuona
kwamba huu ni muda muafaka wa kuingia makubaliano nasi, tunawashukuru
sana kwa kutambua ubora wa huduma zetu, tunawaahidi kwamba wagonjwa
watakaofika kwetu tutahakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati kama
ambavyo mnatarajia” alisema Dkt. Boniface
Dkt Boniface amesema kwamba huduma
zinazopatikana MOI kwa sasa ni sawa na zile zinazotolewa katika mataifa
yaliyoendelea hivyo wagonjwa kutoka Zanzibar watapata huduma nzuri tena
kwa wakati.
” Ndugu Katibu Mkuu tumeboresha
sana huduma zetu, tuna kitengo cha kisasa cha radiolojia, maabara na
wodi za kisasa (Executive ) hivyo tunaamini wagonjwa kutoka Zanzibar na
watanzania wataendelea kupata huduma bora katika Taasisi yetu” Alisema
Dkt Boniface
Hatua hii itapelekea wagonjwa
kutoka Visiwani Zanzibar kupata huduma za kibingwa katika Taasisi ya MOI
na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikitumika
kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.
Tukio hilo limeshuhudiwa na
Mwanasheria wa MOI bwana Suleiman J. Mgerwa pamoja na mwanansheria wa
Wizara ya Afya Zanzibar Bi Shufaa Nassoro Ali, Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar imeamua kurasimisha ushirikiano na Taasisi ya MOI kwani imekuwa
ikitumia gharama kubwa kupeleka wagonjwa nje ya nchi wakati huduma hizo
zinapatikana hapa Tanzania.
No comments:
Post a Comment