Pages

Thursday, January 31, 2019

KATIBU MKUU MADINI AMSIMAMISHA KAZI AFISA DODOMA


AKITAFAKARI JAMBO
Waziri wa Madini Doto Biteko akitafakari jambo wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika eneo ambalo shughuli za uuzaji  wa madini zinafanyika bila kuwa na leseni. Mbele ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila. Wengine ni Maafisa wa Wizara.
MUUZAJI 1
Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati akimhoji Munuzi wa Madini Matondo Michembe (wa pili kulia) ambaye alikutwa akifanya shughuli hizo bila kuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo. Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Doto Biteko.
WAZIRI AKIELEZA JAMBO
Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati alipotembelea kiwanda cha kuchenjua madini ya dhahabu cha Umoja eneo la Viwanda la Kizota wakati wa ziara yake ya kushtukiza. Katikati kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, wengine ni Watumishi wa kiwanda hicho kushoto, Katikati mwenye suruali ya blue ni Afisa aliyesimamishwa kazi, Fundi Sanifu Asheni Daudi, anayefuatia ni Afisa Madini wizara ya madini, Mhandisi Assah Mwakilembe.
………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila amemsimamisha kazi Fundi Sanifu wa Madini, Asheni Daudi wa Ofisi ya Madini Dodoma baada ya kuagizwa na Waziri wa
Madini Dotto Biteko.
Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri Biteko akiongozana na Katibu Mkuu na Wataalam wengine wa wizara vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, kufanya ziara ya kushtukiza katika Kiwanda cha Kuchenjua madini ya Dhahabu cha  Umoja kilichopo eneo la Viwanda la Kizota (Industrial Area) na kubaini mapungufu makubwa katika utendaji kazi wa wataalamu hususan uandaaji wa tarifa za uzalishaji wa madini.
Akizungumza katika eneo hilo, Waziri Biteko alisema wizara ilipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu mienendo inayoendelea katika eneo hilo ambapo wahusika ambao ni Maafisa Madini wamekuwa hawatoi taarifa halisi za uzito na ubora wa dhahabu zinazozalishwa baada ya kuchenjuliwa, hivyo, serikali kukosa mapato stahiki.
Waziri Biteko ameongeza  kuwa, tayari anayo majina yote ya wanaofanya michezo ya ujanja ujanja kwenye viwanda vya kuchenjua dhahabu, huku akieleza kuwa, hatua madhubuti zitachukuliwa kwa wote wanaofanya vitendo hivyo na kuongeza kwamba, zoezi hilo litakuwa endelevu kwa lengo la kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwataka maafisa madini kuwa makini.
“Nakuagiza Kamishna wa Madini David Mulagwa kufanya kaguzi katika viwanda vyote vya kuchenjua dhahabu kwa lengo la kubaini utendaji wa kazi wa viwanda hivyo, ikiwemo taarifa za uzalishaji zinazotolewa na Lazima tufike mahali tuheshimu taratibu, madini haya ni mali ya nchi”, alisema Biteko.
Wakati huo huo, Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkoa wa Dodoma Jonasi Mwano kujitathmini kutokana na mambo yanavyokwenda katika eneo lake la kazi na kumtaka kuwasilisha kwa Kamishna wa Madini na kwa Waziri wa Madini taarifa za uzalishaji madini ya dhahabu kwa kipindi cha miezi sita.
Pia, katika ziara yake, Waziri Biteko alibaini mnunuzi wa madini ya dhahabu katika eneo la Kizota aliyefahamika kwa jina la Matondo Michembe ambaye anafanya shughuli hizo bila kuwa na leseni ya biashara ya madini hayo. Hivyo, alimwagiza Michembe kuwasilisha taarifa za utendaji wake kwa Kamishna wa Madini na Waziri wa Madini hususan  soko analouzia madini  hayo ya dhahabu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila ameelezea kuwa, kiutaratibu ilikuwa lazima taarifa za uzalishaji na kiasi kilichozalishwa kujazwa katika vitabu maalum ndani ya kiwanda hicho lakini jambo hilo halikufanyika kama inavyotakiwa.
Aidha ameongeza kuwa, Afisa huyo amesimamishwa ili kupisha uchunguzi na endapo itabainika, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa.

No comments:

Post a Comment