WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa
amesema amefarijika na maendeleo ya ujenzi wa viwanda kwenye mkoa wa
Tanga kwa sababu vitasaidia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.
Aliyasema hayo jana jioni
(Alhamisi, Novemba 1, 2018) alipotembelea kiwanda cha saruji cha
Rhino
na kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh, vyote vya jijini Tanga.
Waziri Mkuu ambaye jana
alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga,
aliwapongeza wawekezaji wa viwanda hivyo kwa kuunga mkono mkakati wa
Serikali.
Alisema Serikali ya awamu ya
tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kukuza uchumi
kutoka wa chini hadi wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda.
Akizungumzia kuhusu kiwanda
cha Rhino, Waziri Mkuu alisema kiwanda hicho na vingine vya saruji
nchini vitasadia kupunguza gharama ya saruji nchini na kurahisisha
ujenzi.
“Serikali inaamini kwamba
uwepo wa viwanda mbalimbali nchini si tu utawezesha ukuaji wa uchumi wa
Taifa, pia utasaidia katika kumaliza changamoto ya ajira hususani kwa
vijana.”
Akiwa katika kiwanda cha Tanga
Fresh, Waziri Mkuu aliwataka wafugaji mkoani Tanga wabadili mfumo wa
ufugaji na wafuge kwa kutumia njia za kisasa ili waongeze uzalishaji.
“Wafugaji lazima wakubali
kubadilika watumie fursa ya uwepo wa kiwanda hiki kwa kufuga kisasa ili
wapate maziwa mengi kwa sababu wana uhakika wa kuyauza kiwandani hapa”.
Kadhalika, Waziri Mkuu
aliwataka wananchi walioajiriwa kiwandani hapo wafanye kazi kwa bidii,
uaminifu na wawe waadilifu na wasijihusishe na vitendo vya wizi kwa kuwa
havina tija.
No comments:
Post a Comment