Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto)
akizungumza na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali yanayuhusu
Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini na
ameziagiza NGOs kuleta taarifa za fedha za mwaka 2016 na 2017 na
utekelzaji wa miradi yake kwa ofisi ya
Msajili ndani ya siku 30 . Picha
na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW.
Na Mwandishi Wetu Dodoma.
Septemba, 28, 2018
Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeyaagiza
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuwasilisha kwa Msajili wa
Mashirika hayo taarifa za fedha zilizokaguliwa za mwaka 2016 na 2017
ndani ya siku thelathini kuanzia leo Septemba, 28, 2018.
Hayo yamesemwa
leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali yanayuhusu Usajili na
Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.
Dkt. Ndugulile
ameyataka pia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwasilisha taarifa
inayoonesha miradi iliyotekelezwa kwa fedha iliyopatikana kwa mwaka wa
2016 na 2017 na kutoa taarifa ya vyanzo vya mapato husika ikiambatana na
hati za makubaliano za vyanzo husika kwa kipindi cha miaka hiyo.
Naibu Waziri Dkt.
Ndugulile ameeleza kuwa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
ya mwaka 2001 inasisitiza misingi ya uwazi na uwajibikaji kwa Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali nchini.
Amesisitiza kuwa
kwa mujibu wa Kifungu cha 29(a) na (b) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali, Na. 24 ya mwaka 2002, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana
wajibu wa kuwasilisha taarifa za kazi na fedha kila mwaka kwa Msajili
wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kwa Umma.
Ameongeza kuwa
Kanuni za utendaji za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2008
zinasisitiza uzingatiaji wa misingi ya uwazi na uwajibikaji katika
utendaji kazi, masuala ya fedha na utawala hivyo wanufaika wa miradi
yao, Halmashauri wanapofanya miradi na vyombo vya habari wana haki ya
kupata taarifa hizo.
Dkt. Ndugulile
ameeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa miongozo hiyo bado Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali mengi yamekuwa yakikiuka matakwa husika hivyo kuleta
mkanganyiko katika jamii.
“Serikali
itaendelea kufuatilia na haitosita kuchukua hatua kali za kisheria
ikiwemo kuzifutia usajili NGOs ambazo zitashindwa kutekeleza agizo hili
ndani ya muda uliopangwa” alisisitiza Dkt. Ndugulile.
Pia Dkt.Ndugulile
ameziagiza NGOs nchini zizingatie ushiriki wa wazawa wa ndani katika
miradi wanayoitekeleza kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu za
uendeshaji wa shughuli za NGOs hapa nchini.
Aidha Dkt.
Ndugulile ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutuma taarifa zao za
fedha na za miradi kila mwaka kama ilivyoagizwa kupitia barua pepe
ifuatayo dngo@communitydevelopment.go.tz .
Maagizo haya kwa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanakuja siku chache mara baada ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, JInsia,
Wazee na Watoto (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto) Dkt. John Jingu kufuatilia utendaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali nchini wakati alipokuwa akimuapisha kuwa Katibu Mkuu huyo
katika Ikulu ya Chamwino Dodoma.
No comments:
Post a Comment