Pages

Friday, September 28, 2018

IKU YA KIMATAIFA YA WAZEE KUADHIMISHWA KITAIFA MKOANI ARUSHA


DSC_0156
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Nchini Dkt. Naftali Ng’ondi akiwa na Kamishna Msaidizi Bw. Rabikila Mushi (katikati) pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii Bi. Rehema Kombe wa mwanzo kushoto na Irene Kombe Afisa Ustawi wa Jamii jiji la Arusha  akiongea na vyombo vya habari kuhusu maandalizi ya  Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani yatakayofanyika jijini Arusha tarehe 1/10/2018.
DSC_0161
Na Mwandishi Wetu. Arusha. 
Umoja wa Mataifa umetenga kila tarehe 1 Oktoba  kuwa Siku ya Kimataifa ya Wazee kwa lengo la kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili ili kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi maisha ya heshima, hadhi na kuthaminiwa utu wao.  

Haya yamesemwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi wakati wa wa kikao chake na waandishi wa habari mjini Arusha ili kuifahamisha Jamii juu ya Maadhimisho ya  Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani. 
Kamishina Ng’ondi amesema Itifaki ya Haki za binadamu ya Afrika kwa watu wazee ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2016 pamoja na mambo mengine, imesisitiza kuwa kila mmoja anayo haki ya kufurahia haki na uhuru unaotambuliwa na itifaki hiyo bila vikwazo vyovyote kama vile rangi, ukabila, jinsia, lugha, dini, siasa au wazo, mali na utaifa au jamii yake mahali pa kuzaliwa au hali nyingine. 
‘’Ni kwa mantiki hiyo basi Kiongozi wa Dini Nchini Afrika ya Kusini Askofu Desmond Tutu aliwai kusema kuwa, jinsi tunavyozeeka, haki zetu hazizeeki  kwa hiyo ni wajibu wetu kuhakikisha wazee wetu Nchini wanaishi maisha mazuri na yakuheshimika’’. Alisema Dkt. Ng’ondi. 
Kila mwaka Maadhimisho haya hubeba Kaulimbiu yenye ujumbe mahsusi. Kwa mwaka huu 2018, kaulimbiu inasema “Wazee ni Hazina ya Taifa: Tuenzi Juhudi za Kutetea Haki na Ustawi Wao’’. Kaulimbiu hii inahimiza Serikali na Jamii kwa ujumla kutambua na kuenzi jitihada za Wazee katika ujenzi wa Taifa letu. 
Dkt. Ngondi alisisitiza kuwa sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 inahimiza kuwatambua wazee kama rasilimali muhimu katika maendeleo yetu,kuwashirikisha wazee katika maamuzi muhimu yanayowahusu wao na Taifa kwa ujumla na kuwashirikisha katika uzalishaji mali na kuondoa umasikini miongoni mwao. 
Aidha alisema  Sera hiyo pia inasisitiza kuboresha huduma zinazotolewa kwa wazee, kutoa ulinzi wa kisheria kwa wazee kama kundi maalumu na kuwaelimisha vijana kuhusu masuala ya uzee na kuzeeka na kuwajengea uwezo wa kufanya maandalizi ya maisha kuelekea uzeeni. 
Kamishna huyo alitoa wito kwa jamii kuwa haina budi kuenzi na kudumisha mila na desturi nzuri za kuwaenzi wazee kwa kutambua kuwa wazee ndio chanzo  cha urithi wa historia ya nchi, washauri wa familia na jamii, watu wenye hekima na walezi katika Taifa. 
Na pia Kamishna huyo ameitaka jamii kuwa na wajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee katika kupata huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na afya, matunzo na ulinzi katika kipindi chote cha maisha yao.  
Maadhimisho haya kwa mwaka 2018 yanafanyika Kitaifa katika Jiji la Arusha na Mgeni Rasmi katika maadhimisho haya anatarajiwa  kuwa  Mzee wetu Ally Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani ni moja ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) katika kutambua na kuhamasisha Serikali za Nchi Wanachama na wadau wengine kuweza kulinda na kutetea haki za Wazee duniani kote. 

No comments:

Post a Comment