Pages

Thursday, July 19, 2018

Waziri apongeza utendaji mgodi makaa mawe

PichaGreyson Mwase, Songea
NAIBU Waziri wa Madini, Dotto Biteko amepongeza utendaji kazi wa mgodi wa kuzalisha makaa ya mawe wa Kambas uliopo wilayani Songea mkoani Ruvuma na kuitaka migodi mingine nchini kuiga mfano kwenye uchimbaji madini kutoka kampuni hiyo.

Biteko amesema hayo katika ziara yake katika mgodi huo uliopo kijiji cha Maniamba wilayani Songea, Ruvuma kukagua uchimbaji madini pamoja na kutatua changamoto zilizopo.
Aliambatana na wataalamu kutoka Wizara ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, maofisa Madini wa Songea, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Songea.
Baada ya kupokea taarifa ya uchimbaji madini katika mgodi huo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa mgodi huo, Yahya Yusuph Kambaulaya, Biteko aliupongeza mgodi huo kwa kuzalisha makaa ya mawe na kuuza ndani ya muda mfupi tangu imeanza uchimbaji Desemba mwaka jana.
Aliutaka mgodi huo kuunganisha leseni zake 14 za madini ili kuwa na wachimbaji wa kati na wakubwa na kuzidi kuongeza mapato Serikalini.
“Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2017 ni rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Ndani ya kipindi kifupi wameanza kuchimba kwa mafanikio makubwa, kutoa ajira kwa wazawa na kushiriki katika shughuli za huduma za jamii. Nazitaka kampuni za madini nchini kuiga mfano wa kampuni hii,” amesema Biteko.
Amesema, anatarajia kuona mgodi wa Kambas unakua na kuitaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Halmashauri ya Songea na Ofisa Madini wakiulea mgodi huo kwa kufuata sheria.
Biteko alitaka halmashauri kutumia fedha za mapato ya mgodi huo kwa uwekezaji mbadala wa shule, vituo vya afya na barabara ili kuacha kumbukumbu nzuri katika vizazi vijavyo.
Katika hatua nyingine, Biteko aliutaka mgodi wa Kambas kulipa kodi stahiki serikalini baada ya kuuza katika kituo cha mwisho badala ya mauzo ya hapo hapo mgodini (net back value).
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme amempongeza Waziri Biteko kwa usimamizi makini wa sekta ya madini nchini akisema, ofisi yake ipo tayari kushirikiana na mwekezaji huyo pamoja na kutatua changamoto zitakazojitokeza.
Akiwasilisha taarifa ya uzalishaji, Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Kuzalisha Makaa ya Mawe wa Kambas, Yahya Kambaulaya amesema, uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi huo umekuwa ukiongezeka siku hadi siku ambapo mpaka sasa wameshachimba tani 5,138.
Amesema, tani hizo zilichimbwa kwa miezi mitatu, Desemba 2017, Mei, 2018 na Juni, 2018 na Januari hadi Aprili, 2018 uchimbaji makaa ya mawe ulisimama kutokana na mvua kubwa.
Amesema, kuanzia Julai 2018 uzalishaji wa makaa ya mawe kwa siku ni tani 200 na malengo ya mgodi ni kuzalisha tani 600 hadi 700 kwa siku ambapo kwa mwezi mgodi utakuwa na uwezo wa kuzalisha kati ya tani 18,000 hadi 21,000.
Akielezea manufaa ya mgodi wa Kambas, Kambaulaya amesema mgodi umeweza kulipa serikalini kodi mbalimbali inayotokana na mauzo ya makaa ikiwa ni pamoja na mrabaha na ada ya ukaguzi Sh milioni 16, sh milioni 4.1 katika kijiji cha Maniamba za huduma za jamii.

No comments:

Post a Comment