Pages

Friday, July 20, 2018

Watoto 140,000 hawapo shule Zanzibar

PichaKhatib Suleiman, Zanzibar
UTAFITI uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Zanzibar, umebaini kuwa watoto 140,000 wenye umri kuanzia miaka minne hadi 15, wapo nje ya shule kwa sababu mbalimbali.

Sera ya Elimu Zanzibar inawataka watoto wote kuanzia miaka minne hadi mitano kuandikishwa katika shule za maandalizi, elimu ya msingi kuanzia miaka sita hadi 11 na sekondari miaka 12 hadi 15.
Akizungumza katika mkutano wa kutoa mafunzo ya kuandaa mkakati wa kuwarejesha shule watoto waliopo nje yanayofanyika katika kituo cha walimu wa maandalizi (MECP-Z) mjini Zanzibar, Meneja wa taaluma Sharifa Majid, ameyataja makundi matatu ya watoto wanaokosa masomo.
Makundi hayo ni ya watoto ambao hawajawahi kuhudhuria kabisa shule, waliokwenda shule na kutoroka kwa zaidi ya miezi mitatu na wale wasiohudhuria masomo mfululizo kwa mujibu wa utaratibu.
Meneja huyo alisema tafiti zinaonesha kuwa, wengi wa watoto walioko nje ya shule ni kuanzia miaka 12 hadi 15 ambapo baadaye wengine hulazimika kuanza masomo wakiwa na umri mkubwa.
Aidha alisema watoto wa kiume ndio wanaoongoza kwa idadi kubwa kuwa nje ya shule ikilinganishwa na wanawake. Sharifa alizitaja sababu zinazowakosesha watoto elimu kuwa ni umasikini, uelewa mdogo wa wakuu wa familia pamoja na kuishi vijijini ambako baadhi ya wazazi hawajafanya bidii ya kutosha kuhakikisha watoto wanasoma.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, mkufunzi wa walimu wa miaka miwili Safia Salum Mohammed, alisema tafiti zinaonesha kuwa watoto wanaomudu kukamilisha elimu ya msingi ni asilimia 85 ya watoto wote wanaoandikishwa, wakati sekondari ni asilimia 54 ya wale wanaoanza.
“Tumegundua shule nyingi za Unguja na Pemba hazina miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, hivyo kupata wakati mgumu wa kusoma huku vifaa vya kusomea ikiwa ni moja ya kikwazo kikubwa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Unicef kwa kushirikana na Madrasa Zanzibar (MECP-Z), wanafadhili mradi wa kuwashajihisha wazazi kuwaandikisha watoto waliofikisha umri wa kuanza shule pamoja na kuwarejesha waliotoroka, kwa kuwashirikisha masheha.
Kiasi cha Sh milioni 332 zitatumika kugharamia mradi huo wa miaka miwili utakaohusisha shule kadhaa za Wilaya ya Magharibi 'B', ambapo Unicef itatoa asilimia 66 na MECP-E asilimia 33.

No comments:

Post a Comment