TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kuzindua
huduma mpya ya kliniki ya moyo inayotembea (Cardiac Mobile Clinic)
kwa kufuata wagonjwa popote pale walipo na kuwahudumia. Huduma hii maalum
inatarajiwa kuzinduliwa mkoani Ruvuma tarehe 23/7/2018.
Kuanzishwa kwa huduma hii kutasaidia wananchi wengi hasa wa
mikoani ambako ni mbali na Taasisi yetu ilipo kufikiwa kwa urahisi zaidi na
kupata huduma za matibabu ya moyo ya kibingwa.
Baada ya kufanyika kwa uzinduzi huo tutaendelea kutoa huduma kwa
wananchi wa mkoa wa Ruvuma kwa muda wa siku sita kuanzia tarehe
23-28/7/2018. Huduma hii ya kliniki inayotembea itakuwa endelevu katika mikoa
yote ya Tanzania Bara na Visiwani. Siku za karibuni tutatoa ratiba kamili kadri
ya maombi yatakavyotufikia kutoka Tawala za Mikoa.
Huduma tutakazozitoa ni kutoa matibabu baada ya kufanya vipimo kwa
kutumia mitambo mahususi tuliyokuwa nayo. Ushauri wa kiafya kuhusiana na
Magonjwa ya Moyo, elimu ya lishe bora, kutoa Rufaa ya moja kwa moja kwa
wagonjwa watakaokutwa na matatizo ya Moyo kuja kwenye Taasisi yetu
kwa uchunguzi wa tiba zaidi.
Dhumuni la Taasisi ni kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma bora
na kuwa na elimu inayohusiana na magonjwa ya Moyo. Wananchi wote wa mkoa
wa Ruvuma pamoja na mikoa ya jirani tunawakaribisha mfike katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma (Songea) ili muweze kupata huduma za uchunguzi na
matibabu ya moyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete
20/07/2018
No comments:
Post a Comment