Albano Midelo
TANZANIA imebahatika
kuwa na viumbe adimu duniani ambao wanavutia watalii kila kona ya dunia.
Moja ya vivutio hivyo ni mjusi ambaye anafahamika kwa jina la Tendaguru
anayepamba makumbusho ya Ujerumani.
Tendaguru ni mjusi mkubwa kuliko hata
tembo ambaye anaaminika kuwa ndiye mnyama mwenye umbo kubwa wa nchi kavu
na mnyama mwenye uzito mkubwa, aliyehifadhiwa katika Makumbusho ya
viumbehai ya Berlin, Ujerumani. Mjusi huyo alivumbuliwa katika eneo la
Tendaguru mkoani Lindi miaka 100 iliyopita. Mjusi huyo ambaye ana uzito
wa tani 50 ni kivutio adimu katika makumbusho ya Berlin, Ujerumani.
Mjusi huyo kwa jina la kitaalamu anaitwa dinosaur ambapo masalia ya
mjusi huyo katika eneo la Tendaguru, yalikusanywa na kupelekwa Ujerumani
ambako wataalamu waliyaunda na kisha kuyaweka kwenye Makumbusho ya
Berlin yaliyojengwa tangu mwaka 1889.
Tendaguru ndilo jina ambalo linatumiwa na
watafiti na wataalamu katika machapisho yaliyopo kwenye makumbusho hayo
ambapo wanalitumia jina hilo kutambulisha mijusi wote wakubwa sio wa
Tanzania pekee bali pia wanaotoka katika nchi nyingine. Mjusi huyo
anakadiriwa kuwa na umri wa miaka milioni 150, ana urefu wa meta 13.7
kwenda juu, anakadiriwa kuwa na moyo wenye uzito wa kilo 400 na chakula
cha mjusi huyo kilikuwa ni mimea.
Mwanasayansi wa mambo ya kale, Dk Daniella
Schliart anasema mjusi huyo aligundulika kati ya mwaka 1907 na 1909
ambapo watafiti katika eneo la Tendaguru walikuwa wanatafiti madini
ndipo walikutana na masalio hayo kisha kukusanya masalia na
kuyasafirisha hadi nchini Ujerumani. Wanasayansi hao na watafiti
walibaini kuwepo aina 13 tofauti za mijusi ambao baadhi yao waliishi kwa
kula mimea na wengine nyama.
Dk Schliart anabainisha namna walivyopata
umri wa mjusi huyo ni kwa kuangalia makundi ya madini yalivyopangiliwa
na kwa kutumia programu za kompyuta. Masalio ya mjusi huyo yanatunzwa
kwa kutumia kemikali maalumu za kumlinda asije akasambaratika. Naibu
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa kimataifa na Sayansi, Dk
Christopher Hauser anasisitiza kuwa Tanzania inahitaji wataalamu wa
mambo kale ambao wamepata mafunzo maalumu ya kuhudumia masalia ya mijusi
wa kale.
“Tanzania itayarishe wataalamu wa kutunza
masalia ya mijusi kwa sababu wanakaa miaka mingi hivyo wanaweza
kuharibika. Utafiti unaonesha kuwa bado Tanzania kuna masalio ya mijusi
katika eneo la Tendaguru na maeneo mengine,’’ anasisitiza Dk Hauser.
Licha ya kuhifadhiwa masalia ya mjusi huyo kutoka Tanzania katika
Makumbusho ya Ujerumani kuna masalia ya viumbe wengine ambao ni nyoka,
ndege, simba, chui na mijusi wakubwa kutoka nchi mbalimbali. Makumbusho
ya nchini Ujerumani yapo chini ya Wizara ya Elimu na Utafiti ambayo
huingiza wastani wa watu 500,000 kwa mwaka ambapo kiingilio chake ni
euro nane kwa kila mtu anayetembelea makumbusho hayo.
Nchi ya Ujerumani na Tanzania
zimekubaliana kuendeleza tafiti za masalia ya mijusi katika eneo la
Tendaguru. Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya
Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi mapema mwaka huu
kutembelea Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin,Ujerumani.
Meja Jenerali Milanzi aliongoza msafara wa
Tanzania ulioshiriki maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya ITB Berlin 2018
yaliyofanyika Ujerumani yakishirikisha taasisi tano za serikali na
kampuni binafsi 60 kutoka Tanzania. Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya
Ujerumani, Profesa Johannes Vogel alimueleza Meja Jenerali Milanzi kuwa
shughuli kubwa inayofanywa na makumbusho hiyo ni utafiti kwa ajili ya
maendeleo ya sayansi, elimu na ufahamu wa mambo mbalimbali kuhusu dunia.
Akizungumzia fursa zilizopo za
kushirikiana kutafiti maeneo yaliyogundulika masalia ya mijusi hao na
viumbe wengine, Profesa Johannes alisema makumbusho yake yapo tayari
kushirikiana na wanasayansi wa Tanzania ili kujenga uwezo wa kufanya
utafiti na kupata matokeo yatakayochangia katika hazina ya maarifa na
sayansi ya viumbe na mazingira. “Masalia ya mjusi huyu yachukuliwe kuwa
urithi wa dunia nzima na hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha urithi huu
hauachwi ukapotea. Hivyo, ni vema tukaimarisha utafiti katika eneo
walikopatikana ili kupata masalia mengi zaidi na kuitangaza Tanzania
katika nyanja za utafiti," anasisitiza profesa huyo.
Anasema Makumbusho ya Ujerumani ipo tayari
kufanya ziara ya kuimarisha mazungumzo na mamlaka za Tanzania ili
utafiti katika eneo la Tendaguru uendelee kwa manufaa ya Tanzania na
dunia nzima.Kwa upande wake, Milanzi aliahidi kutoa ushirikiano ili
kuwezesha tafiti hizo kufanyika Tanzania kwa ajili ya ustawi wa sayansi
na uchumi wa nchi zote mbili. Makumbusho ya Berlin ina mikusanyo mingi
ya viumbe mbalimbali zaidi ya milioni 30 ikiwemo ya mijusi kutoka nchi
nyingine duniani. Mkusanyiko huo kwa pamoja unatoa mvuto kwa watafiti na
watalii kutembelea na kufanya shughuli zao chini ya makumbusho hiyo.
Kuendelea kuwepo masalia ya mjusi huyo
katika makumbusho hiyo kuna manufaa zaidi ya kuitangaza Tanzania
kiutalii na utafiti wa kisayansi kuliko masalia hayo kurejeshwa nchini
Tanzania kwa kuwa mjusi huyo ni balozi wa utalii na utafiti wa kisayansi
anayeitangaza Tanzania sehemu mbalimbali duniani.
Makala imeandikwa kwa msaada
wa mitandao na Albano Midelo ambaye ni mchangiaji wa gazeti hili.
Mawasiliano yake ni albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917.
No comments:
Post a Comment