Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akisisitiza kuhusu umuhimu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa
Sheria, Kanuni na Taratibu na kuepuka vitendo vyote vya kuwabugudhi
wafanyabiashara wakati wa kutekleza jukumu la kukusanya kodi katika
maeneo yote nchini wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa
Waziri Mkuu leo Bungeni Jijijni Dodoma.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akisisitiza jambo wakati akijibu
miongozo ya wabunge leo Bungeni Jijini Dodoma mara baada ya kipindi cha
maswali na majibu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na
matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 leo Bungeni Jijini
Dodoma.
Sehemu ya wageni waliofika bungeni wakifuatilia kipindi cha maswali na majibu leo Bungeni mjini Dodoma.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji
Mhandisi Isack Kamwelwe akitoa maelezo kuhusu hatua zinazochukuliwa na
Serikali katika kufikisha huduma za maji kwa wananchi kote nchini.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii
Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza kuhusu taratibu za
matibabu hasa kuhusu kitendo cha baadhi ya viongozi kuonyesha mfano
katika kutoa chanjo cha wasichana wenye umri wa miaka kuanzia 14 ili
kuzuia saratani ya mlango wa kizazi wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.
Mbunge wa viti maalum (CCM) Mhe.
Amina Mollel akisisitiza kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika
kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanajengewa mazingira rafiki
yatakayowawezesha kushiriki katika ujenzi wa uchumi.
( Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO
………………..
Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kukaa pamoja na chama cha wapangaji wa
nyumba za
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kusikiliza changamoto zao pamoja na
kutoa fursa kwa wapangaji wa muda mrefu kununua nyumba hizo.
Mhe. Majaliwa ametoa tamko hilo
leo Bungeni, Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ilala
Mhe. Azzan Mussa Zungu juu ya lini Serikali itakutana na wanachama na
wamiliki wa nyumba za NHC ili kutoa fursa kwa wapangaji wa muda mrefu
kuzinunua nyumba hizo badala ya kuwaondoa.
“Shirika la nyumba inayo sera
inayotoa muongozo namna nyumba hizo zinavyotakiwa kutumika ikiwemo na
maamuzi kwa wale wanaokaa kwa muda mrefu kwenye nyumba hizo inapofikia
thamani ya nyumba kushuka iweze kurasimishwa rasmi ili kutoa fursa kwa
wapangaji hao kuweza kuzinunua kwa kulipa kiwango kidogo kidogo,”
alisema Waziri Mkuu.
Aliendele kusema, asilimia kubwa
ya wapangaji wa muda mrefu wa nyumba hizo ni wastaafu ambao hawana
nyumba. Hivyo ameitaka NHC kuangalia jambo hilo na kuwapa fursa
wapangaji hao kulipa kidogo kidogo kadiri ya uwezo wao.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotumia lugha ya kuudhi au
kutumia nguvu pindi wanapokusanya kodi kwa wafanyabiashara. Badala yake
wawaelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kulipa kodi na kuwaeleza
ni kwa kiasi gani kodi hiyo imefikia.
Amesema hayo, alipokuwa akijibu
swali la Mbunge wa Jimbo la Tunduma Mhe. Frank Mwakajoka kuhusu kauli ya
Serikali juu ya usumbufu unaoletwa na TRA kwa wafanyabiashara wakati wa
kukusanya kodi.
“Serikali imeunda chombo cha
kusikiliza kero za wananchi ndani ya TRA lakini kama hawatasikilizwa
wanauwezo wa kupeleka kero zao Wizara ya Fedha au kwa kiongozi yoyote
mkubwa katika eneo lake kama vile Mkuu wa Mkoa au Wilaya,” alisema
Waziri Mkuu.
Aidha ameitaka Mamlaka hiyo
kufanya kazi kwa weledi na kuwa na mazungumzo na wafanyabiara. Pia
tathmini ya kodi isiwe kiwango kikubwa kuliko mtaji wa mfanyabiashara.
Hata hivyo amesema hatua
zitachukuliwa kwa yeyote ambaye hatatumia utaratibu mzuri wa kukusanya
kodi na amewataka wafanyabiashara kufanya biashara kwa amani.
No comments:
Post a Comment