Na Veronica Kazimoto,
Tanga,
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani
Tanga imekamata majahazi manne yenye bidhaa mbalimbali katika Kijiji cha
Kigombe wilayani Muheza kwa kupitia njia ya magendo zikitokea visiwani
Zanzibar.
Akizungumza
hivi karibuni baada ya kukamata majahazi hayo, Meneja wa Forodha kutoka
TRA mkoani hapa Edward Ndupa alisema kuwa, bidhaa zilizokamatwa ni
pamoja na tani 5 ya sukari, vitenge, khanga na mafuta ya kupikia madumu
470 ya lita 20 kila moja.
“Tumefanikiwa
kukamata majahazi manne yakiwa na tani 5 za sukari, vitenge, khanga
pamoja na mafuta ya kupikia madumu 470 ambapo thamani ya bidhaa zote
hizo ni takribani shilingi milioni 35”, alisema Ndupa.
Ndupa
ameeleza kuwa, mpaka sasa wafanyabiashara wenye bidhaa hizo
hawajafahamika hivyo, Mamlaka inafanya utaratibu wa kuzitaifisha moja
kwa moja.
Naye
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP) Edward Bukombe amewataka wafanyabiashara wote wanaojihusisha na
biashara za magendo kuacha mara moja vitendo hivyo na kuongeza kuwa,
jeshi hilo litaendelea kushirikiana na TRA kwa ajili ya kuwakamata
wale wote wanaosafirisha bidhaa kupitia njia sizizo rasmi.
“Natoa
wito kwa wafanyabiashara wote wanaokwepa kulipa kodi na kupitisha
bidhaa zao katika njia za magendo kuacha mara moja tabia hiyo. Sisi kama
Jeshi la Polisi, tumejipanga vizuri na tutaendelea kushirikiana na
Mamlaka ya Mapato Tanzania kuwabaini na kuwakamata wafanyabiashara
wanaokiuka sheria ikiwa ni pamoja na kukamata bidhaa husika,”
Alisisitiza Bukombe.
SACP
Edward Bukombe amewahimiza wafanyabiashara kufuata sheria, kanuni na
taratibu ili waweze kufanya biashara zao bila kubughudhiwa na hatimaye
waweze kujiingizia kipato kilicho halali.
No comments:
Post a Comment