Mkurugenzi
Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati
akifungua mjadala wa wadau wa maendeleo ulioshirikisha wawakilishi
kutoka taasisi za umma na Serikali na asasi za kiraia kujadili uchambuzi
uliofanywa na taasisi hiyo kuangalia sera, mikakati na mipango ya
Serikali kumuwezesha mwanamke kuelekea uchumi wa viwanda.
TGNP Mtandao imekutanisha wajumbe
kutoka makundi mbalimbali ya wadau wa maendeleo wakiwemo wawakilishi
kutoka taasisi za umma na Serikali na asasi za kiraia kujadili uchambuzi
uliofanywa na taasisi hiyo kuangalia sera, mikakati na mipango ya
Serikali
kumuwezesha mwanamke kuelekea uchumi wa viwanda.
Akizungumza wakati akifungua
majadiliano, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi leo
jijini Dar es Salaam amesema taasisi hiyo imefanya uchambuzi wa sera,
mikakati na mipango ya Serikali kuangalia ushiriki wa wanawake na
makundi mengine ya pembezoni katika Tanzania ya viwanda.
Alisema katika uchambuzi huo
uliofanywa na Profesa Flora Kessy, Mtafiti wa TGNP umeangalia maeneo
mbalimbali ikiwemo changamoto za kundi la wanawake linavyoweza
kushirikishwa kwa mafanikio ya Tanzania ya viwanda.
Akifafanua zaidi, Bi. Liundi
aliwataka wajumbe hao kujadiliana kwa kuzingatia kuwa takwimu za ‘UN
Women’ zinaonesha mwanamke ni uti wa mgongo wa maendeleo kutokana na
kuchangia takriban kwa asilimia 43 katika nguvu kazi duniani na kwa nchi
nyingine asilimia hiyo inafikia hadi 70.
Alisema kwa upande wa Tanzania
kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 65.5 ya Watanzania huku idadi kubwa
ya kundi hilo wakiwa ni akinamama, jambo ambalo linaonesha upo umuhimu
mkubwa wa kundi hilo kuangaliwa kipekee katika uwezeshwaji kufikia
malengo kuelekea uchumi wa viwanda.
Hata hivyo alisema bado kuna
changamoto nyingi katika kundi la wanawake kuelekea uchumi wa viwanda,
ukizingatia kundi kubwa la wanawake liko katika sekta isiyo rasmi
(asilimia 51.1), idadi ndogo ya wanawake wanaomiliki ardhi (asilimia 8)
ukilinganisha na wanaume, idadi kubwa ya wanawake kuwa katika kundi la
umasikini (asilimia 60) ukilinganisha na wanaume.
“…Jinsia ni suala la Maendeleo
hatuna budi kwa pamoja kutoa kipaumbele ili kuongeza ushiriki wa
wanawake wenye tija katika maendeleo ya uchumi wa nchi. Ni wazi kuwa
mkutano huu utatumika kujadili kwa kina na kupanga mikakati ya
kuimarisha ushiriki wa wanawake pamoja na sera hizo bado kuna changamoto
ya utekelezaji ili kuwezesha ushiriki wenye tija kwa wanawake na
makundi ya pembezoni,” alisema Bi. Liundi.
“Katika kusisitiza ushiriki wa
Wanawake katika Tanzania ya Viwanda tuzingatie kanuni (principle) ya
malengo endelevu ya dunia ya kutomwacha mtu nyuma kwa kufanya uchambuzi
wa kina kwa jicho la jinsia ili kuleta ushiriki jumuishi na wenye tija.
Ikumbukwe kwamba tukiacha kundi la wanawake nyuma tunapoteza fursa na
mapato kwa kiasi kikubwa hivyo kutuchelewesha kufikia uchumi wa kati na
dira yetu ya 2025,” alisema.
Kwa upande wake Mtafiti Prof.
Kessy akiwasilisha uchambuzi kwa washiriki hao alibainisha kuwa shughuli
wanazozifanya akinamama kwa sasa zinaweza kuboreshwa zaidi kulingana na
mahitaji hivyo kujikuta kundi hilo linajengewa uwezo.
Alisema shughuli kama uzalishaji
mdogo mdogo unaofanywa na kundi hilo unaweza kuongezewa teknolojia,
masoko pamoja na nguvu za uzalishaji na kukuta inamuinua mwanamke na
kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda.
Kundi hilo kwa pamoja litajadili
na kuchakata changamoto hizo na kutoka na mapendekezo ambayo watajaribu
kuishirikisha Serikali kupitia wizara husika ili kuona uwezekano wa
kuzingatiwa kwa mapendekezo ya wadau hao.
No comments:
Post a Comment