Mwenyekiti wa Jumuiya ya taasisi
ya vyuo vya elimu ya juu Tanzania (TAHLISO) akisoma tamko la Marais wa
Vyuo vikuu katika mkutano uliofanyika leo Chuo Kikuu cha Dodoma(Udom),
Mjini Dodoma
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Marais wa Vyuo Vikuu Nchini wakishiriki mjini Dodoma leo.
………………..
Jumuiya ya Taasisi za Vyuo vya
Elimu ya Juu Tanzania(TAHLISO)imeyaonya wanaotumia kifo cha Mwanafunzi
Akwilina Akwilini kisiasa huku wakitumia mwamvuli wa jumuiya hiyo kutoa
matamko mbalimbali waache tabia hiyo vinginevyo watachukuliwa hatua.
Aidha, Jumuiya hiyo imewaomba
wanafunzi kuendelea kuwa watulivu kusubiri matokeo ya
uchunguzi wa kifo
cha Akwilina na kujiepusha na maandamano na vitendo vyovyote vya
uvunjifu wa amani.
Onyo hilo limetolewa leo mjini
Dodoma na mwenyekiti wa jumuiya hiyo, George Mnali alipokuwa akizungumza
na vyombo vya habari wakati wa kikao na kamati tendaji ya Tahliso kwa
ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu
nchini.
Kikao hicho kimehusisha Marais wa serikali za wanafunzi wa Vyuo hivyo nchini.
Mnali amesema Tahliso ndio chombo kikuu cha kuwasemea wanafunzi wote nchi nzima na sio kikundi kingine chochote.
“Vipo vikundi vingi vimejitokeza
na kutoa matamko mbalimbali baada ya kifo hiki cha Mwanafunzi mwenzetu
Akwilina Akwilini kutokea, vikundi vingine vikaenda mbali zaidi kwa
kuwataka baadhi ya watendaji wa serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya
Ndani Kujiuzulu jambo ambalo linaashiria vikundi hivyo kutumika
kisiasa,”amesema
Ameeleza kuwa haiwezekani kutaka
watendaji wa serikali wajiuzulu wakati uchunguzi bado unafanyika na
matokeo ya uchunguzi bado hayajatoka.
“Jambo la kusikitisha zaidi kuna
baadhi ya vikundi vimejitangaza kwamba vinaungwa mkono na Marais wa Vyuo
Vikuu jambo ambalo sio la kweli,”amesema Mwenyekiti huyo
Ametoa wito kwa vikundi vyote
vinavyojihusisha na kutumia mwamvuli wa Marais wa Vyuo Vikuu kama kinga
yao ilikuuhadaa umma kwamba wanaungwa mkono, viache tabia hiyo
vinginevyo watachukuliwa hatua.
Hata hivyo amesema Tahliso
wanasubiri matokeo ya uchunguzi unaofanyika juu ya kifo cha Akwilina na
wanatumai wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amewaomba wanafunzi waendelee kuwa
watulivu wakati wanasubiri matokeo hayo nakujiepusha na maandamano na
vitendo vyovyote vinavyosababisha uvunjifu wa amani na kuleta mgawanyo
miongoni mwa wanafunzi.
Kadhalika, amesema namna bora ya
kufikisha hoja ni kutumia njia ya majadiliano kama wasomi badala ya
kutumia nguvu ya maandamano kwa kutofuata taratibu na madhara yake ni
kusababisha vurugu zisizotakiwa na hatimaye kuhatarisha usalama na hivyo
kuathiri jamii kwa ujumla wake.
Mnali amemshukuru Rais John
Magufuli kwa kuingilia kati suala hilo la kifo cha Akwilina na kuagiza
uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote
watakaobainika kuhusika na kifo hicho.
No comments:
Post a Comment