Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akielezea jambo mbele ya
Wadau wa Afya, mashirika yasiyo Yakiserikali, na Serikali katika kikao
kilichofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar
es salaam.
Afisa kutoka kitengo cha Elimu ya
Afya kwa umma Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Amalbega Kasangala akiwasilisha taarifa mbele ya mgeni rasmi
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy
Mwalimu(hayupo kwenye picha).
Wadau wa Afya, mashirika yasiyo
Yakiserikali, Watumishi wa Serikali na Waandishi wa Habari wakifuatilia
taarifa kutoka kwa mgeni rasmi Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu(hayupo
kwenye picha), katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa
Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.
………………
Na WAMJW.
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kuwa na watoa
huduma wa Afya ngazi ya jamii (CHWz) Zaidi ya 30,000 ifikapo mwaka 2020
katika vijiji Zaidi ya 15,000 nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu
katika Mkutano wa Wadau wa Afya, mashirika yasiyo Yakiserikali, na
Serikali katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar
es salaam.
“Tunataka itakapofika mwaka 2020,
tuwe na angalau Wahudumu wa Afya zaidi ya 30,000 katika vijiji Zaidi ya
15,000 tulivyonavyo Tanzania, Eneo hili tumeliona ni eneo muhimu
kwasababu tutapata matokeo ya haraka, ni bora kutumia Bilioni 40 kwa
ajili ya kinga ya magonjwa kwa Watanzania .” Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
Mhe. Ummy alisema kuwa lengo la
Mkutano huo ni kujadiliana na Wadau wa Maendeleo na Mashirika yasiyo
Yakiserikali juu ya kuimarisha huduma ya Afya ya msingi hasa katika
kuwakinga wananchi dhidi ya maradhi kupitia mikakati ambayo inakubalika
kimataifa ya kuwa na watoa huduma katika ngazi ya jamii.
“Kisera tumesema kuwa tunataka
kuwa na watu wawili ambao watakuwa wanafanya kazi kama watoa huduma za
Afya na kazi yao kubwa haitakuwa kutibu bali itakuwa ni kusisitiza
masuala ya lishe, masuala ya uzazi wa mpango, kuhimiza watu kujua hali
zao hasa katika maambukizi ya VVU na kuwaelekeza waende maeneo gani ili
kupata huduma za Afya” alisema Mhe. Ummy
Kwa upande mwingine Mhe. Ummy
Mwalimu aliwashukuru wadau wa maendeleo na Mashirika yasiyo Yakiserikali
kwa kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kufanikisha kuwa na
watoa huduma za Afya ngazi ya jamii kwa idadi yakuridhisha ifikapo 2020.
Hata hivyo Waziri Ummy alisema
kuwa rasilimali watu katika Sekta ya Afya nchini ni Asilimia 51, huku
kukiwa na upungufu wa watoa huduma za Afya kwa Asilimia 49, ambao ni
pamoja na Madaktari, Wauguzi, Wataalamu wa Maabara, huku mikoa ambayo
inaupungufu Zaidi ni Katavi, Rukwa, Tabora, Kigoma na Kagera.
Naye, Afisa kutoka kitengo cha
Elimu ya Afya kwa umma Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Dkt. Amalbega Kasangala alisema Serikali kuwa Serikali
imejipanga katika kukinga ugonjwa kuliko kutibu jambo ambalo litasaidia
katika kupunguza gharama kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment