Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Open Heart
International (OHI) ya nchini Australia tumefanya upasuaji wa
kufungua kifua kwa wagonjwa 16 wenye matatizo ya Moyo. Kati ya hao watoto ni tisa na watu wazima saba .
Upasuaji
huu umefanyika katika kambi maalum ya matibabu ya Moyo iliyoanza tarehe
25/11/2017 na kumalizika leo tarehe 01/12/2017.
Wagonjwa
watu wazima tumewafanyia upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu
kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass Grafting) na kubadilisha
milango ya moyo miwili hadi mitatu iliyokuwa imeziba au haifungi vizuri.
Kwa upande wa watoto tumefanya
upasuaji na vipimo kwa watoto ambao vyumba vyao vya moyo havijakamilika
na hivyo damu kwenda kwa wingi kwenye mapafu. Kuwafanyia watoto vipimo
tukiwa tumefungua vifua inasaidia kufahamu aina ya upasuaji tunaotakiwa
kuufanya.
Upasuaji tuliowafanyia watoto ni
wa awali ili kuutayarisha moyo kwa ajili ya upasuaji mwingine ujao.
Watoto waliofanyiwa upasuaji katika kambi hii ni wenye uzito wa kuanzia
kilo nne hadi 12 ambao umri wao ni miezi minne hadi miaka minne.
Kwa mara ya kwanza tumeweza
kufanya upasuaji kwa mtoto ambaye moyo wake ulikuwa upande wa kulia na
vyumba vyote vya moyo vinafanana wakati vinatakiwa kuwa tofauti . Katika
upasuaji huu tumeweza kulinda mapafu yalikuwa yanapokea damu kwa wingi
kutoka kwenye mishipa ya moyo. Mtoto huyu pia tumeweza kumuwekea kifaa
ambacho kitamsaidia moyo wake kufanya kazi vizuri (Pace Maker).
Kwa
namna ya kipekee tunawashukuru sana wenzetu hawa wa OHI kwa kuona
umuhimu wa kushirikiana na sisi kutoa matibabu kwa wagonjwa wenye
matatizo ya moyo. Pia wamekuwa wakitoa mafunzo kwetu ambayo yametusaidia
sana kuongeza ufanisi wa kazi. Kabla ya kuanza kambi hii kulikuwa na
mafunzo kwa wauguzi wetu ambao walifundishwa jinsi ya kuwahudumia
wagonjwa waliopo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU).
Aidha tunawaomba wananchi
waendeleee kuchangia damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo
wanahitaji kuongezewa damu wakati wanapatiwa matibabu. Kwa mtu mmoja
mmoja au kikundi cha watu wanaopenda kuchangia damu tunawaomba wafike
Taasisi ya Moyo iliyopo Muhimbili mkabala na Maabara kuu. Kwa maelezo
zaidi wawasiliane kwa simu namba 022-2151379 au 0713304149.
Naomba
nimalizie kwa kuwahimiza wananchi ambao bado hawajajiunga na mifuko ya
bima ya afya waweze kujiunga kwani matibabu hasa ya moyo gharama zake ni
kubwa. Kujiunga na mifuko ya bima ya afya kutawasaidia kulipia gharama
za matibabu pindi watakapougua.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano na Masoko
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
01/12/2017
No comments:
Post a Comment