Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maagizo kuhusu matumizi ya fedha za
kigeni katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza kuwa
utekelezaji wake uanze tarehe 1 Januari, 2018. Maagizo hayo ni kama
ifuatavyo: –
- Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za ...vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.
- Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.
- Viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.
- Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.
Aidha Dkt. Mpango ameviagiza
vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika
kukiuka maagizo haya ya Serikali.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
No comments:
Post a Comment