MAOFISA kutoka Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Zanzibar wakikagua eneo linalotarajiwa kujengwa
kiwanja cha ndege huko Kigunda Jomba Mkoa wa Kaskazini Unguja.
…………………………………………………………….
Na Salum Vuai, MAELEZO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar
iko katika maandalizi ya ujenzi wa kiwanja kipya kidogo cha ndege
kitakachosaidiana na kile cha Abeid Amani Karume kilichoko Kisauni
Wilaya ya Magharibi ‘B’.
Kiwanja hicho kinatarajiwa
kujengwa kwenye...
kijiji cha Kigunda Mkoa wa Kaskazini Unguja kilichoko
takriban kilomita 50 kutoka mjini Unguja.
(Leo Novemba 4, 2017), Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), ilianza kuwalipa fidia ya mazao
wananchi 99 kutoka shehia za Tazari, Kilindi na Kigunda waliokuwa
wakiendesha shughuli za kilimo katika eneo linalotarajiwa kujengwa
kiwanja hicho.
Kwa mujibu wa ofisa uhusiano wa
mamlaka hiyo Makame Abdalla Seti, takriban shilingi 57,000,000 zimelipwa
kwa wakulima hao baada ya kuvifanyia tathmini vipando vyao kwa
kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na
Uvuvi.
Akizungumza katika hafla ya
uzinduzi wa malipo kwa wakulima hao uliofanyikia ofisi ya Mkuu wa
Wilaya ya Kaskazini ‘A’Gamba, Seti alisema eneo lenye urefu wa kilomita
mbili na upana wa mita 200 limetengwa na mamlaka kwa ajili ya mradi huo
utakaogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alisema kitakapokamilika, kiwanja
hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea ndege mbili ndogo mfano wa ATR 172, C
208, C 172, Bombadier na nyengine zenye uwezo wa kubeba abiria
wasiozidi 50.
Alifahamisha kuwa lengo la ujenzi
huo ni kupunguza msongamano katika uwnaja wa Abeid Amani Karume, na
mzunguko wa safari za watalii ambao kwanza hufika Tanzania Bara au hata
nchi jirani za Afrika Mashariki na baadae kuja hapa Zanzibar.
Alisema watalii hao ni wale
wanaofikia hoteli zilizoko ukanda wa utalii wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,
kwenye maeneo ya Nungwi, Matemwe na Kiwengwa ambako harakati za kitalii
zimeongezeka maradufu.
“Tunajua watalii wengi wanaokuja
nchini mwetu huwa wanataka kupumzika na hawapendi kusafiri masafa marefu
kuzifikia hoteli zao wanazopanga, hivyo kiwanja hichi kitasaidia
kuwafikisha moja kwa moja badala ya kuteremka Kisauni na kupoteza saa
kadhaa barabarani,” alifafanua.
Halikadhalika, alisema iwapo
kutatokezea dharura yoyote itakayozuia matumizi ya uwanja wa sasa,
kiwanja hicho kitatumika kama mbadala kwa kupokea ndege zitakazofika
nchini za kiwango husika.
Ofisa huyo alisema, hatua ya
kwanza ilikuwa kulizuia eneo hilo na inayofuata ni kulisafisha huku
taratibu za kutangaza zabuni kwa wakandarasi zikiendelea kufanyika.
Naye Ofisa Mazingira wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Zanzibar Suleiman Hamad Omar, alitumia fursa hiyo
kuwashukuru wananchi waliokuwa wakitumia ardhi hiyo kwa kuridhia kupisha
mradi huo muhimu kwa maendeleo ya kijiji chao na taifa kwa jumla.
Aidha, alieleza kuridhishwa na
kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya Wilaya kuwatafuta,kuwaorodhesha
wahusika, kuvitathmini vipando vyao na hatimaye kuwezesha kuwalipa
stahiki zao kwa mujibu wa thamani sahihi.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’
Hassan Ali Kombo, alisema ridhaa ya wananchi hao inatokana na kutambua
umuhimu wa miradi ya maendeleo inayoanzishwa na serikali, na mbali ya
kuwashukuru, aliwataka kutumia fedha walizolipwa kutafuta shughuli za
uzalishaji zitakazowainua kisha na familia zao.
Kwa upande wao, wanufaika wa
malipo hayo, wameishukuru serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
kwa kuwapa muda wa kuvuna mazao yao kabla kuanza kuisafisha ardhi hiyo
kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo, na kusisitiza kutoa kipaumbele cha
ajira kwa vijana wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ mradi huo utakapoanza
No comments:
Post a Comment