Wanafunzi wa Chuo cha Kodi (ITA)
jijini Dar es salaam, wametakiwa kutumia vyema teknolojia ya mawasiliano
hususan mitandao ya kijamii kujifunza ili kupata maarifa badala ya
kuitumia kwa mambo ambayo hayatawasaidia katika masomo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa
Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo wakati akiwakaribisha wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga na chuo hicho kwa...
mwaka wa masomo 2017/18.
Amesema vijana wengi wanatumia
mitandao ya kijamii kwa masuala ya kijamii kwa kiwango kikubwa kuliko
kuitumia kujifunza na kupata maarifa kwa mambo ambayo yatawasaidia
kukuza kiwango cha elimu.
“Elimu ipo kila mahali siku hizi:
katika vitabu, mitandao na tuna mambo mengi ambayo yanasaidia sana
kujifunza tofauti na ilvyokuwa miaka 30 iliyopita. Ni wajibu wa
wanafunzi kuitumia vyema mitandao hususan simu kujifunza na kupata
maarifa”, alisema Prof. Jairo.
Mkuu huyo wa chuo amesema kwamba
chuo cha kodi kinatumia mfumo wa kujenga umahiri kwa mwanafunzi ili
aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu na ambao
umelenga kumuwezesha mwanafunzi kujifunza badala ya kufundishwa.
Ameongeza kwamba mfumo huo ndio utaratibu unaotumika ulimwenguni ili
mwanafunzi anapohitimu awe na uwezo wa kujua nini cha kufanya katika
fani yake na kwa Chuo cha Kodi ajue jinsi ya kukusanya kodi.
“Msije mkakaa mkategemea
mtafundishwa tu na mtakaa na kumsikiliza mwalimu, hapana, tunawatarajia
mjifunze kwa kutumia nyenzo mbalimbali zilizopo”, amesema Prof. Jairo na
kuongeza kwamba huo ndio utaratibu unaotumika katika mfumo wa kujenga
umahiri kwa mwanafunzi.
Katika hatua nyingine amewataka
wanafunzi hao wa Astashahada ya Uwakala wa Forodha ya Afrika Mashariki,
Shahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi na Stashada ya Uzamili ya Kodi,
kuzingatia masomo kwani ndio lengo lao kuu la kuomba kujiunga na chuo
cha kodi na kwa upande wake chuo cha Kodi kitatimiza wajibu wake
kuhakikisha wanapata elimu wanayostahili na katika mazingira bora.
Aidha amewahakikishia wanafunzi
hao kwamba wale watakaofaulu vizuri watapata ajira kutoka Mamlaka ya
Mapato Tanzania kwani TRA huchukua wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha
juu.
Kuhusu maisha katika Chuo cha
Kodi, Prof. Jairo amewataka wanafunzi hao kuishi kwa mujibu wa sheria za
nchi pamoja na kufuata sheria ndogo ndogo na taratibu za chuo.
Pamoja na Mkuu wa Chuo cha Kodi,
katika kuwakaribisha wanafunzi hao, pia walikuwepo Kaimu Naibu Mkuu wa
Chuo Taaluma Justin Musa, Kaimu Mkuu wa Chuo, Utawala Emmanuel Masalu,
Mkuu wa Huduma za Fedha Emmanuel Foya, Makamu wa Rais wa Serikali ya
wanafunzi wa Chuo cha Kodi (ITASO) Darafu Abdalah, Wakuu wa vitengo
mbalimbali pamoja na walimu.
No comments:
Post a Comment