NA OWM, MBEYA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali
imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo
mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ilitengewa sh. bilioni
2.72 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji.
Amesema mkakati huo unatekelezwa kupitia
Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, wananchi katika maeneo
yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita
400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumapili,
Julai 30, 2017) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Halmashauri za
Rungwe na Busokelo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale
katika wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
Alisema mkoa wa Mbeya umetengewa sh. bilioni
10.383 kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati
yake sh. bilioni 2.72 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya
maji kwenye wilaya ya Rungwe.
Waziri Mkuu alitaja mradi mwingine
unaotekelezwa wilayani Rungwe ni pamoja na mradi wa maji wa Masoko wenye
thamani ya sh. bilioni 5.3, utakaohudumia jumla ya vijiji 15. “Mradi huu ni
miongoni mwa miradi inayojengwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji
kwa fedha za ndani.”
Alisema mradi huo utakapokamilika
utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika vijiji vya Bulongwe,
Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata,
Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.
Pia Waziri Mkuu alisema wananchi lazima wazingatie sheria ya
Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye
maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza
watendaji kuwachukua hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli
mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya
vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.
“Hatuwezi kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili
ya watu wachache wanaoharibu mazingira kwa kuendesha shughuli za kibinadamu
ndani ya vyanzo vya maji. Ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka
katika vyanzo vya maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria.”
Awali Mbunge wa Jimbo la Busokelo Mheshimiwa
Fredy Mwakibete na mbunge wa Rungwe Mheshimiwa Saul Amon walimueleza Waziri
Mkuu kwamba upatikanaji wa huduma ya maji na salama ni miongoni mwa changamoto
zinazoyakabili majimbo yao.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta jambo na Mbunge wa Mbeya Mjini, (CHADEMA),
Mhe. Joseph Mbilinyi, "Sugu", wakati wa ziara yake mkoani humo, Julai
31, 2017
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Salim Jessa (wanne
kushoto) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Malumalu kilichopo
Iyunga jijini Mbeya wakati alipoembelea kiwanda hichi Julai 31,
2017. Watatu kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea maua kutoka kwa mtoto , Felista (4) wa
Shule ya Wenye Ulemavu ya Child Support Tanzania ya jijini Mbeya baada ya
kuwasili kwenye kiwanda cha vinywaji baridi cha SBS - PEPSI kilichopo eneo la
Iyunga jijini Mbeya Julai 31, 2017.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na watoto wa Shule Wenye Ulemavu ya Child
Support Tanzania ya jijini Mbeya baada ya kuwasili kwenye kiwanda cha vinywaji
baridi cha SBS- Pepsi kilichopo Iyunga jijini Mbeya
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha vinywaji baridi cha SBS-
Pepsi kilichopo eneo la Iyunga jijini Mbeya, Julai 31, 2017.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wakazi wa Mbeya baada ya kuwasili kwenye
Viwanja vya Ruanda Nzove jijini humo kuhutubia mkutano wa hadhara, Julai
31, 2017. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Salim Jessa
(kulia) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Malumalu
kilichopo Iyunga jijini Mbeya wakati alipoembelea kiwanda hicho Julai 31,
2017. Kushoto kwake ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Viwanja vya
Ruanda Nzove jijini Mbeya Julai 31, 2017. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
No comments:
Post a Comment