Pages

Thursday, August 31, 2017

Mfuko wa PPF na mchango wa vifaa tiba vituo vya afya nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Mhe. Jenista Mhagama,(wa tatu kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, (wa pili kushoto), Viongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Longido, wakitembelea wodi ya wagonjwa ya Kituo cha Afya Longido, ambapo ni moja kati ya vituo vilivyonufaika na msaada wa vifaa tiba wa PPF. 

NA CHRISTIAN GAYA. MTANZANIA, ALHAMISI AGOSTI 31, 2017
Sekta ya afya ni miongoni mwa huduma muhimu katika kuhakikisha afya na ustawi wa wananchi. Jamii yenye afya na ustawi mzuri ni muhimu sana katika kuongeza uzalishaji katika ngazi ya...
familia na taifa kwa ujumla.
Taifa lenye nguvu kiuchumi na kimaendeleo hujengwa na jamii yenye afya njema. Kama ilivyo katika Elimu, sekta ya afya imepewa kipaumbele  ambapo utekelezaji umeongeza juhudi za serikali katika sekta ya afya na kuleta matokeo chanya kwa ujumla kitaifa.
Tatizo la ufinyu wa bajeti, hupelekea malengo mengi tarajiwa katika zahanati na vituo vya afya kutotimizwa kama ilivyokusudiwa na upungufu wa wataalamu wa afya mfano madaktari, wauguzi, wakunga, katika ngazi zote za huduma ya afya.
Pia kuna upungufu wa dawa muhimu na vifaa vya tiba na ukosefu wa maabara na miundombinu mingine kama vile umeme, maji, nyumba chache za watumishi. Kuzuia vifo vya mama na mtoto ikiwa ni changamoto inayoikabili sekta ya afya
Wilaya za mijini zinaonyesha kuwa na idadi kubwa ya vituo vya afya angalau kwa kila kata ikilinganishwa wilaya za vijijini. Hii inatokana na kuwa sekta binafsi imekuwa ikijelekeza katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya vingi katika maeneo
ya mijini na kuyasahau maeneo ya vijijini ambako mahitaji yamekuwa makubwa na yakiongezeka siku hadi siku.
Na ndiyo maana Mfuko wa Pensheni wa PPF kulingana na sera yake ya uchangiaji na udhamini mpaka sasa unaendelea kukabidhi vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya nchini.
Mfano katika wilaya ya Kisarawe, Mfuko wa PPF umekabidhi vifaa tiba hivyo kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Utumishi na Utawala bora Mhe. Selemani Jaffo kwa ajili ya hospitali ya Wilaya ya Kisarawe ambavyo ni vitanda 2 vya kujifungulia wakinamama, vitanda 4 vya wagonjwa wa kawaida, mashuka 56 na vifaa vinavyotumika kujifungulia wakinamama.
Wakati anapokea vifaa hivyo, Mhe. Jaffo anasema Mfuko wa PPF walichofanya ni jambo kubwa kwa vile hospitali za wilaya ya Kisarawe zilikuwa zikikabiliwa na changamoto katika sekta ya afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, anasema Mfuko unatoa vifaa tiba hivyo ikiwa ni muendelezo wa zoezi la kurudisha kwenye jamii kulingana na sera ya uchangiaji na udhamini ya PPF.
Vifaa tiba hivyo vyenye jumla ya shilingi 99,983,700/- vilikabidhiwa kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na  Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa PPF wakati wa mkutano wake wa 26 wa Wanachama na Wadau Arusha.
Ambapo wakati wa kufunga Mkutano huo, mgeni rasmi Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu aliungana na Bodi ya Wadhamini wa PPF, Menejimenti na baadhi ya Wafanyakazi wa PPF kwenda kukabidhi vifaa tiba hivyo katika Kituo cha Afya, Longido, ambacho ni moja kati ya vituo vya  Afya 16 nchini vinavyonufaika na  msaada wa vifaa hivyo.
Mhe. Jenista Mhagama, anasema, PPF imefanya jambo zuri la kusaidia jamii na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwapatia huduma bora za afya wananchi wake.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea  www.hakipensheni monitor online na hakipensheni blog Simu +255 655 13 13 41

No comments:

Post a Comment