Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR –
TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo akiiongoza Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali
za Mitaa kukagua ujenzi wa mabweni uliokamilika katika shule ya sekondari ya
Wasichana ya Msalato vipaji maalum Mjini Dodoma.
NA K-VIS BLOG, DODOMA
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo ameambatana na Wajumbe wa
Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kujionea ujenzi wa majengo ya
mabweni ya wanafunzi katika shule ya sekondari Msalato nje kidogo ya Manispaa
ya Dodoma.
Akiongea wakati wa ziara hiyo na kumkaribisha
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jafo amesema
kwamba agenda kubwa ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ni kubadilisha mandhari ya shule
kongwe na kuendelea kuzifanya ziwe bora.
“Sisi tuliopewa dhamana na Mheshimiwa Rais,
katika Ofisi yake, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, katika
fedha zilizotengwa, katika kusimamia miundo mbinu hii, lakini katika agenda
kubwa ya kubadilisha shule hizi kongwe, Mheshimiwa Mwenyekiti naomba
nikuhakikishie tunaifanya kazi hii kwa nguvu zote”
Amesema kuimarika kwa mazingira ya kusomea
kumewavutia wanafunzi wengi ambapo katika kipindi cha likizo ni wanafunzi 50 tu
ndio watakaokwenda likizo lakini takribani wanafunzi 850 hawatakwenda likizo
ili kujisomea shuleni hapo lakini pia amesema Serikali itakuwa na mpango
utakaoandaliwa ili kupata wanafunzi bora watakaojiunga na shule maalum za
vipaji katika kipindi kifupi kijacho kwani kwa sasa kidato cha tano na sita
wamekwisha tumia utaratibu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa Jasson Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini
amesema mpango wa kukarati na kujenga majengo ya shule utaboresha mazingira ya
kusomea, “kuna mpango wa Serikali ya CCM wa kujenga au kukarabati majengo na
miundo mbinu ya shule 88 Tanzania, miundo mbinu hiyo ni pamoja na mabweni,
madarasa, mabwalo, maabara, nyumba za walimu, majengo yote ya shule, vyoo na
kadhalika”
Mhe. Rweikiza amelishukuru Shirika la nyumba
la Taifa(NHC) kwa kujenga majengo yanayokidhi kiwango kinachokubalika na hivyo
kazi kubwa ni kwa wanafunzi kujisomea kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Saada Mkuya amesema mazingira ya kusomea
tayari ni rafiki kwa wanafunzi bali pia maslahi ya walimu yaangaliwe pia.
“Tumeona sasa mazingira ya yamekuwa mazuri mno, kwamba kiasi ambacho kinafanya
wanafunzi wao wenyewe wajisikie wapo vizuri lakini pia maslahi ya walimu katika
mapato yao yafikiriwe”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya
Dodoma Bw. Godwin Kunambi amesema kuwa mazingira ya kusomea yameboreshwa,
madawati pia yapo ikiwemo ya ziada, pia Halmashauri ya Manispaa imetoa gari
shuleni hapo kwa ajili ya usafiri na hivyo anategemea Manispaa ya Dodoma kuwa
miongoni mwa shule bora zitakazotoa wanafunzi wa kumi bora kutoka katika shule
hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo akijibu baadhi ya maswali
kwa wanakamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kukagua ujenzi wa
mabweni uliokamilika katika shule ya sekondari ya Wasichana ya Msalato vipaji
maalum Mjini Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo akitoa hotuba kwa walimu,
wataalam, wanafunzi na wanakamati ya Bunge kabla ya kumkaribisha
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Jasson Rweikiza
aliyekaa kushoto kwake.
No comments:
Post a Comment