Afisa Mwandamizi wa Tathmini ya
Mikopo wa TADB, Bw. Mubezi Buberwa (kulia) akitoa maelezo kuhusu huduma
za mikopo inayotolewa na Benki hiyo kwa Waziri mwenye dhamana ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles Tizeba.
Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa
TADB, Bw. Saidi Mkabakuli (wapili kulia) akizungumza wakati Waziri
mwenye dhamana ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles Tizeba
(kushoto) alipotembelea Banda la TADB.
Waziri mwenye dhamana ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles Tizeba (kushoto) akizungumza na
maafisa wa Benki ya Kilimo juu ya umuhimu wa kuharakisha utoaji wa
mikopo kwa wasindikaji wa maziwa nchini.
Maafisa wa TADB, Bw. Mubezi
Buberwa (kulia) na Bw. Saidi Mkabakuli (wapili kulia) wakimsikiliza kwa
makini Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt.
Charles Tizeba (kushoto) wakati Mhe. Dkt. Tizeba alipotembelea Banda la
TADB siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki ya Maziwa
iliyokuwa ikifanyika Kitaifa mjini Bukoba.
Mhe. Dkt. Tizeba akisisitiza jambo kwa Maafisa wa TADB.
Waziri mwenye dhamana ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles Tizeba (kushoto) akiagana na watumishi
wa Benki ya Kilimo mara baada ya kutembelea Banda la Benki hiyo katika
Viwanja vya Kyakairabwa yaliyopafanyikia Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki
ya Maziwa.
…………………………
Na Mwandishi wetu, Bukoba
Waziri mwenye dhamana ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles Tizeba ameiagiza Benki ya Maendeleo ya
Kilimo ya Tanzania (TADB) kuharakisha kutoa mikopo kwa
wasindikaji wa
maziwa nchi ili kuongeza tija kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini.
Waziri Dkt. Tizeba alitoa agizo
hilo wakati akizungumza na watumishi wa Benki hiyo katika Kilele cha
Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki ya Maziwa iliyokuwa ikifanyika Kitaifa
mjini Bukoba, mkoani Kagera tangu tarehe 28 Mei na kufikia kilele chake
tarehe 01 Juni, 2017.
Dkt. Tizeba alisema utoaji wa
mikopo kwa wasindikaji una umuhimu wa kipekee kwa kuwa utachangia
uhakika wa masoko kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini hali
itakayochochea tija kwa wafugaji hao hivyo kuchagiza lengo la Serikali
la Awamu ya Tano ya kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuweza
kunufaika na sekta hizo.
“Serikali ya Awamu ya Tano
imedhamiria kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi hivyo uanzishwaji wa
Benki ya Kilimo lazima usaidie katika kuhakikisha wasindikaji wa maziwa
wanapata huduma za TADB kwa wakati ili tupate uhakika wa masoko kwa
wafugaji wetu ili tuiinue Tasnia ya Maziwa ili ichangie ukuaji wa uchumi
na maendeleo nchini,” alisema.
Kwa mujibu wa mpango kazi wa TADB,
sekta ya mifugo ni mojawapo ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo
kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika
uongezaji wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa nchini.
Na Benki imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa Ufugaji wa
Ng’ombe wa Nyama na Maziwa ili kuongeza tija kwenye Tasnia za nyama na
maziwa ili kuchagiza maendeleo katika tasnia hizo.
Katika kuhakikisha wasindikaji wa
maziwa wananufaika na huduma za TADB, Benki hiyo inatoa mikopo ya aina
tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya
Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda
Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).
Kwa mujibu wa Mpango Kazi huo,
mikopo hiyo ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na
kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha
kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
TADB ni taasisi ya serikali
ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa
fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini ambao ulikuwa
unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha
kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa; riba kubwa kwenye
mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi; masharti magumu ya kukopa bila
kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo na mazao ambayo inaathiriwa
kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
No comments:
Post a Comment