Pages

Friday, June 2, 2017

MAJALIWA ASHIRIKI SALA YA IJUMAA KWENYE MSIKITI WA AL – GADDAF


ZIL1
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Sheikh Nurdin Kishik ambaye ni Mhadhiri wa Kimataifa wa Dini ya Kiislaam, (kulia) na ujumbe wake, ofisini kwake bungeni mjini Dodoma  Juni  2, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
ZIL2
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kushiriki katika sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa  Al- Gadaf mjini Dodoma Juni 2, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuliombea Taifa ili liendelee kudumu katika hali ya amani na utulivu.
Amesema suala la kudumisha amani na utulivu ni jukumu la kila mmoja, hivyo kila
mwananchi kwa imani yake ahakikishe anashiriki kutunza hali hiyo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 2, 2017) baada ya kumaliza kuswali sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Gadaf, mjini Dodoma.
Amesema ni vema kila mwananchi akajivunia hali ya amani na utulivu iliyoko nchini kwa kuwa ndiyo inayowezesha kufanyika kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo. “Tuendelee kudumisha amani, tufanye ibada kila mtu kwa imani yake. Serikali inaheshimu dini zote kwa sababu ndizo zinazojenga amani na mshikamano,” amesema.
Pia amewataka wazazi wahakikishe wanawalea watoto wao katika mazingira ya kidini ili wanapokuwa watu wazima waje kuwa raia wema. “Tuendelee kuhamasisha watoto wetu wasikilize mahubiri ya dini; ni jukumu letu sisi kama wazazi kuwahimiza wahudhurie mahubiri ya viongozi wa dini ili waweze kujijenga vyema kimaadili na kiimani pia.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewakumbusha Waislamu wahakikishe wanautumia vizuri mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kuzidisha ibada na kusaidia watu wenye mahitaji. “Leo ni Ijumaa ya kwanza katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, nawaomba tutumie vizuri mwezi huu ili tupate baraka,” amesema.
Ibada hiyo ya sala ya Ijumaa iliongozwa na Sheikh Nurdin Kishki ambaye ni Imamu wa Msikiti wa Vetenari, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.
Sheikh Kishki katika hotuba yake, aliwasisitiza Waislamu waendelee kufanya mambo mema yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu ikiwemo kuwatunza wazazi wao, kumswalia Mtume Mohammed (S.A.W) na kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.

No comments:

Post a Comment