Waziri wa Katiba na Sheria, Prof.
Palamagamba Kabudi ametembelea Ubalozi wa Tanzania Nairobi Kenya na
kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania Nchini Kenya Mheshimiwa Balozi
Mteule Dkt. Pindi Hazara Chana. Prof. Kabudi alifanya ziara hiyo tarehe
4/5/2017 wakati akihudhuria Mkutano wa 56 wa Mwaka wa Jumuiya ya
Mashauriano ya Masuala ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika
(Asian-African Legal Consultative Organisation –AALCO) unaofanyika mjini
Nairobi.
Katika ziara hiyo Prof. Kabudi
aliongozana na Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda Balozi Mteule wa
Tanzania Nchini India yalipo makao makuu ya Jumuiya hiyo na maafisa
wengine wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Prof. Kabudi alimpongeza Balozi
Pindi Chana kwa uteuzi na alishukuru kwa maandalizi waliyoyafanya
kuhakikisha ujumbe wa Tanzania unashiriki ipasavyo mkutano huo. Vile
vile alimuhakikishia kuwa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na taasisi
zake zitampa ushirikiano stahiki katika utekelezaji wa majukumu yake, na
kwamba Ubalozi uwe tayari kwa kufuata taratibu zilizopo kiserikali
kuwasiliana na Wizara pindi yanapoibuka masuala yanayohitaji ushiriki wa
Wizara.
Kwa upande wake Balozi Dkt. Pindi
Chana alimshukuru Prof. Kabudi kwa kutenga muda kuja kuutembelea
Ubalozi na kumpongeza kwa uteuzi alioupata. Balozi Chana alimuahidi
Prof. Kabudi kuwa Ubalozi utaendelea kushirikiana ipasavyo na Wizara kwa
kutumia taratibu zilizopo utahakikisha kuwa masuala ya Wizara
yanaifikia Wizara kwa wakati.
No comments:
Post a Comment