WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali ina mkakati wa kufanya yote nchini yawe na barabara za viwango
vya kimataifa na zinazopitika kwa urahisi.
“Tumeanza kujenga barabara za kisasa
katika jiji la Arusha ambalo ni jiji la utalii, tutakwenda Mwanza na Dar
es Salaam kwa kujenga barabara zenue njia za juu (flyovers) zikiwemo za
magari na
za waenda kwa miguu,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Alhamisi, Mei 4, 2017) wakati akizumngumza na wananchi wa Tengeru,
wilayani Arumeru, mkoani Arusha mara baada ya kukagua barabara ya
Sakina-Tengeru yenye urefu wa km. 14.1 ambayo itakuwa na njia nne za
magari.
“Nimekuja kukagua ujenzi wa barabara
hii ya Sakina hadi Tengeru lakini mkandarasi akimaliza anajenga barabara
nyingine ya kilometa 42.1 na hivyo hapa Arusha tutakuwa na kilometa
56.5 za awamu ya kwanza,” alisema.
Alisema maboresho ya barabara za Jiji
la Arusha yanafanyika ili kuwezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa
zao kwa urahisi na viwanda vitakapoanza kujengwa, itakuwa hawana shida
ya mawasiliano.
Akizungumzia tatizo la uhaba wa ardhi
aambalo lililibuliwa na mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari,
Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw, Mrisho Gambo
aendelee na zoezi la kuuzungukia mkoa wake ili kubaini maeneo yenye
matatizo sugu.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa
barabara hiyo kwa Waziri Mkuu, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha,
Eng. Mgeni Mwanga alisema ujenzi wa barabara hiyo ambao ulianza Juni
2015, unatarajia kukamilika Juni 2018.
“Ujenzi wa barara ya Sakina –Tengeru
ni wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa km. 230 ya
kutoka Arusha –Holili- Taveta –Voi ambayo ujenzi wake unatarajiwa
kugharimu sh. bilioni 139.34. Ujenzi huo unagharimiwa na Serikali ya
Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Sambamba na barabara hiyo, Eng. Mwanga
alisema mkandarasi wa barabara hiyo ataanza kujenga barabara nyingine
ya km. 42.1 inayoanzaia Usa River hadi Kisongo kwa kiwango cha lami
ambayo itakuwa na madaraja saba wakati ile ya Sakina hadi Tengeru ina
madaraja makubwa mawili.
Naye mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw.
Joshua Nassari alisems uhaba wa ardhi bado ni tatizo kubwa kwenye wilaya
hiyo kiasi kwamba hawana hata eneo la kujenga shule au zahanati.
“Maeneo yote yameuzwa na wenyeviti wa
vijiji na madiwani, hivi sasa ukitaka kujenga shule au zahanati hakuna
eneo hata moja. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba utusaidie kufuatilia
suala hilo licha ya kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi
alishakuja na kuelezwa hali halisi ilivyo,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MEI 4, 2017.
No comments:
Post a Comment